HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA DAR ES SALAAM,
TAREHE
22 DESEMBA, 2014
Shukrani
Mheshimiwa
Makamu wa Rais;
Mheshimiwa
Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi
wa CCM Mkoa;
Viongozi
Wenzangu;
Viongozi
wa Dini;
Wazee
Wangu;
Wananchi
Wenzangu;
Nawashukuru sana wazee wangu wa Dar es Salaam,
kwa kukubali mwaliko wangu na kuja kuzungumza nami siku ya leo. Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya muda mfupi, lakini
mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki.
Naomba radhi kwamba ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje
ya uwezo wangu, tukaahirisha mpaka leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu.
Kama mjuavyo, kila ninapoomba kukutana nanyi
ninalo jambo au mambo muhimu kitaifa, ambayo napenda kuzungumza nanyi, na kwa kupitia
kwenu, taifa zima linapata habari. Leo
nina mambo mawili:
Wazee
Wangu;
Kwanza kabisa, nataka kurudia kuwashukuru
Watanzania wenzangu kwa moyo wenu wa upendo, mliouonyesha kwangu katika kipindi
chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli
nina deni kubwa kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba
watu wamekuwa wananiombea uponyaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na
kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana
kuifanya afya yangu, kuendelea kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo
ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Ndugu
Wananchi;
Jambo la kwanza ninalotaka kulizungumzia leo
ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba,
2014 na jana tarehe 21 Desemba 2014 katika maeneo ambayo uchaguzi huo,
uliahirishwa. Bila ya shaka sote,
tumesikia taarifa ya awali ya zoezi la upigaji kura iliyotolewa na Mheshimiwa
Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tarehe 17 Desemba,
2014. Katika taarifa yake hiyo,
Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi limeenda vizuri kwenye maeneo
mengi nchini. Uchaguzi ulifanyika kwa
ukamilifu katika Halmashauri 141
kati ya 162. Katika Halmashauri 21 uchaguzi wake
uliahirishwa na umefanyika jana tarehe 21 Desemba, 2014.
Kwa jumla, katika maeneo mengi uchaguzi
ulifanyika kwa salama na amani na hivyo kuwapa wananchi fursa ya kuchagua
viongozi wanaowapenda kuongoza vijiji vyao, vitongoji vyao na mitaa yao. Kufanyika kwa uchaguzi huu ni uthibitisho
mwingine wa kuendelea kukomaa kwa demokrasia nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za
dhati kwa wale wote walioshiriki katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama vya
siasa na wagombea. Natoa pongezi maalum
kwa walioshinda. Nawaomba sasa wakae
chini kutengeneza mikakati na mipango ya kuwaongoza wananchi wa maeneo yao
katika kupata ufumbuzi wa changamoto za maendeleo na za maisha zinazowakabili.
Ndugu
wananchi;
Katika taarifa yake hiyo pia, Waziri Hawa
Ghasia alielezea masikitiko yake kuhusu kasoro za uendeshaji wa zoezi
zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali.
Aidha, aliahidi kuchukua hatua stahiki za kinidhamu dhidi ya watendaji
na viongozi wa Serikali waliosababisha kasoro hizo. Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza
kuchukuliwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi, kushushwa cheo,
kukatwa mshahara au kupewa onyo.
Napenda kuelezea kufurahishwa kwangu na
msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na nampongeza kwa hatua alizochukua. Namuunga mkono na namtaka aendelee na msimamo
huo katika kukabili vitendo vya utovu wa nidhamu wa watumishi wa umma. Lazima kila mtumishi wa umma, ajue kuwa
asipotimiza ipasavyo majukumu yake, kuna adhabu inayolingana na kosa
alilofanya. Isitoshe, watu hao ndio watakaoendesha
na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakiwa mawakala na wasaidizi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi. Hivyo basi, kuwajibishwa
wale waliozembea katika uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na kwa wengine katika
uchaguzi wa mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.
Ndugu
wananchi;
Kwa upande wa ghasia, fujo na ugomvi uliotokea
wakati wa zoezi la uchaguzi, nimezungumza na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi
na kuwataka kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo vya kuvunja sheria, wanatiwa
nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Nimewataka wasifanye ajizi na watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari ambao hawana budi kuchukuliwa
hatua thabiti za kuwadhibiti na kuwaadabisha. Tusipofanya hivyo, tunawakatisha
tamaa raia wema na watiifu wa sheria. Aidha,
watu wakikamatwa na kuachiliwa muda mfupi baadae, wakati mwingine hata bila
dhamana ya namna yo yote inawachanganya sana watu wema. Isitoshe tutakuwa tunalea maradhi ya watu
wabaya na kuwafanya waendelee kusumbua jamii.
Nimewakumbusha kuwa wasipokuwa wakali sasa, tunaweka mazingira ya hatari ya kuja kutokea
mambo mabaya zaidi mwaka ujao kwenye
uchaguzi mkuu.
Sakata
la Akaunti ya Tegeta ESCROW
Ndugu
Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia si
geni masikioni kwenu, nalo ni sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya
shaka mtakumbuka kuwa wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014,
kulitolewa madai kuwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta
iliyoko Benki Kuu zimechotwa kinyemela na mmiliki wa Kampuni ya Pan African
Power Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa wa Serikali.
Serikali iliahidi kufanya mambo mawili.
Kwanza, kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye
ukaguzi wa Akaunti hiyo na kwamba taarifa yake itawasilishwa Bungeni. Na, pili, kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa
mwenendo mzima wa miamala katika Akaunti hiyo na kama kuna uhalifu wo wote uliopo
kwenye mamlaka yake, achukue hatua zipasazo kwa mujibu wa mamlaka na madaraka
aliyonayo.
Ndugu
Wananchi;
Yote mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali amefanya ukaguzi wa miamala katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko
Benki Kuu na taarifa yake ilishawasilishwa Bungeni. Pia niliagiza taarifa hiyo ichapishwe kwenye
magazeti na tovuti ya Serikali ili watu waweze kuisoma. Agizo hilo nalo limetekelezwa.
TAKUKURU wameendelea na uchunguzi wao na
watakapomaliza na kuridhika kuhusu makosa yaliyofanywa, watawafikisha wahusika mahakamani. Mkurugenzi Mkuu wa PCCB alifika kwenye Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala
hili, aliyoyaona ni muhimu Kamati iyajue.
Mambo
Manne Makuu
Ndugu
Wananchi;
Tarehe 8 Desemba, 2014 nilipoanza kazi
baada ya mapumziko ya ugonjwa, nilikabidhiwa taarifa mbalimbali kuhusu sakata
hili. Tangu wakati huo nimekuwa nazisoma
pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali na kuagiza nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali
kutoka kwa wahusika. Shabaha yangu ni
kuyaelewa vizuri mambo hayo ili niweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wa
uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu
manne:-
(a) Akaunti ya ESCROW
(b)Miliki ya PAP kwa IPTL
(c) Kodi
za Serikali, na
(d)Tuhuma za Rushwa
Akaunti
ya ESCROW
Ndugu
Wananchi;
Katika Mikataba ya Kununua Umeme (Power Purchase Agreements) ambayo
TANESCO imetiliana sahihi na kampuni binafsi za kuzalisha umeme za IPTL,
SONGAS, SYMBION POWER na AGGRECO, kuna malipo ya namna mbili yanayofanywa na TANESCO.
Kwanza, hulipia umeme ilionunua kutoka kwa
kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy
charges). Na, pili hulipia gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo,
yaani tozo ya uwekezaji (capacity charges).
Katika mikataba yote hiyo imekubaliwa kuwa iwapo kutatokea kutofautiana, au
mzozo unaohusu uwekezaji, upo utaratibu wa usuluhishi. Utaratibu huo unataka
kwanza kufanyike mazungumzo, wakishindwa kuelewana watafute mtu wa kuwashauri
na kuwasuluhisha; wakishindwa kukubaliana wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama)
cha Kimataifa cha Usuluhisi wa Migogoro ya Uwekezaji (International Centre for
Settlement of Investment Disputes – ICSID) kilichopo London, Uingereza
Ndugu
Wananchi;
Mwaka 1998 TANESCO walifikisha kwenye Kituo
cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko
kwamba gharama za uwekezaji za IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi
walichowekeza. Mwaka 2001 Kituo cha
Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo.
Madai ya TANESCO yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola za Marekani 127 na siyo Dola milioni 163.17 walizodai
IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa
gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity
charges) nayo ilipunguzwa kutoka Dola
za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji
wa tozo hiyo.
Ndugu
Wananchi;
Miaka minne baadaye TANESCO ilianza vuguvugu
la kutaka kupata nafuu zaidi. Waliamua
kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka 2001. Nimeambiwa kuwa wanasheria wa TANESCO
walishauri Shirika hilo lidai ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa IPTL ufanyike
kwa kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi 50,000 badala ya kutumia
msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola
za Marekani milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1.
Wakati wakisubiri mchakato wa usuluhishi wa
mzozo huu mpya kuanza, pande zote mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti ya Escrow
ya Tegeta. Tarehe 5 Julai, 2006 akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa
sahihi na IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO
upande mwingine. Aidha, Benki Kuu
iliteuliwa kuwa wakala wa kutunza akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.
Ndugu
Wananchi;
Kwa mujibu wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL
iliendelea kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika
kulipa madai hayo. Malipo hayo
yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta tofauti na ilivyokuwa
kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa moja.
Utaratibu huu mpya ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili zitakapofikia
mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji.
Kwa upande wa malipo ya gharama ya umeme (energy charges), TANESCO imeendelea kulipa moja kwa moja kwa IPTL
bila kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na mgogoro.
Ndugu
Wananchi;
Kwa miaka saba tangu tarehe 5 Julai, 2006,
akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka tarehe 5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi
shughuli zote za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kutafuta
ufumbuzi wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na TANESCO. Pande mbili husika hazikuwahi kukaa
kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji kama ilivyofanyika mwaka 1998.
Wakati wote huo, TANESCO iliendelea kulipa
madai ya tozo ya uwekezaji ya IPTL na kupeleka malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji ulisimama katika kipindi kifupi wakati
kampuni ya IPTL ilipowekwa kwenye ufilisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti hiyo inafungwa tarehe 20
Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi
8,020,522,330.37; Hatifungani zenye thamani ya shilingi 159,231,370,000 na Dola
za Marekani 22,198,544. Fedha zote hizo ni sawa na shilingi bilioni 202.9.
Ndugu
Wananchi;
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kama TANESCO
ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo, wakati huo Akaunti hii ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati
Akaunti inafungwa TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni 103.8.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa
riba ya asilimia mbili ya fedha zote
ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo
basi, riba iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za Marekani milioni 33.6.
Ni matumaini yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa
katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka
kumbukumbu sawa na sahihi kuhusu kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya
ESCROW siku uamuzi wa Mahakama ulipofanya akaunti hiyo ifungwe. Kwa kifupi, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali inaeleza kuwa Akaunti hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi bilioni 306.7 kama inavyodaiwa
na baadhi ya watu.
Fedha
za Nani
Ndugu
Wananchi;
Ni matumaini yangu pia kwamba maelezo
haya kwa kiasi fulani yamesaidia kutoa jibu kwa swali maarufu la fedha za
kwenye akaunti hii ni za nani? Je ni za umma
au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea
Akaunti ya ESCROW ni nini? Akaunti ya
ESCROW ni tofauti na akaunti nyingine tunazozijua katika Benki zetu ambazo mtu
anaweka fedha zake. Kama tujuavyo,
katika Benki zipo Akaunti za aina tatu ambazo wengi tunazifahamu na kuzitumia
yaani Akaunti ya Akiba (Savings Account), Akaunti ya Hundi (Current Account) na
Akaunti ya Muda Maalum (Fixed Deposit Account).
Akaunti ya Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa ajili ya kufanya
kazi maalum, kwa masharti maalum na kazi hiyo ikiisha akaunti yenyewe
hufungwa. Akaunti hiyo husimamiwa na wakala
aliyeteuliwa kwa makubaliano ya wale wanaofungua akaunti hiyo. Wakala ndiye mwenye jukumu la kusimamia
akaunti na kumlipa mwenye fedha wakati ukifika.
Kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta pande mbili husika zilikubaliana kuwa
Benki Kuu ndiyo iwe Wakala. Ni muhimu
kujua kuwa akaunti hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye Benki yoyote, siyo lazima
BoT.
Akaunti ya Tegeta ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka
2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges) zilizokuwa zinalipwa
na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa ambaye ni IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja
kwa moja kwa IPTL. Kama nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili
kutoa nafasi kwa pande hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango
cha tozo ya uwekezaji ya IPTL.
Kimsingi basi, fedha hizi ni za IPTL kwani
ndiye mlipwaji na ni malipo yanatokana na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo
ya uwekezaji. Hata hivyo, kwa mujibu wa
CAG, inawezekana katika fedha hizo kuna fedha za umma. Hi ni kwa namna mbili.
Kwanza, kama
mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha tozo ya uwekezaji kupungua
kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika ICSID-1 na kama pande mbili husika
zingekubaliana au kuagizwa kuwa punguzo hilo lianze kuhesabiwa tangu tarehe ilipofunguliwa
Akaunti hiyo (tarehe 5 Julai, 2006), basi kungekuwepo pesa za kurejeshwa
TANESCO. Maadamu hili halikufanyika mpaka Mahakama
ilipofanya uamuzi uliosababisha akaunti hiyo kufungwa. Katika mazingira hayo fedha zote zinakuwa ni za
IPTL maana hakuna madai ya TANESCO.
Ndugu
Wananchi;
Namna ya pili ni ile ambapo katika fedha hizi,
kunaweza kuwepo fedha za umma na iwapo kuna kodi za Serikali ambazo
hazijalipwa. Kwa mujibu wa Taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuthibitishwa na TRA ni
kwamba kulikuwa na kodi ya VAT ambayo haikulipwa. Nimeambiwa kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu
wa kukata kodi hizo kabla ya kulipa madai ya IPTL, lakini kwa baadhi ya malipo
haikufanyika hivyo. Hivi IPTL inastahili
kudaiwa kodi ya Serikali? Kwa mujibu wa
tathmini iliyofanywa, kodi inayotakiwa kulipwa na IPTL ni shilingi bilioni 21.7. IPTL wameshapelekewa madai na TRA, na IPTL wamekubali
kulipa.
Katika ukaguzi wa Hesabu za TANESCO za mwaka
2012, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliwaelekeza TANESCO
kuacha kuhesabu fedha zilizopo kwenye Akaunti ya ESCROW kama ni fedha zao. CAG aliwaambia TANESCO kwamba fedha hizo si
zao.
Maagizo hayo ya CAG yanasomeka kama ifuatavyo:
“As a result, the
deposit balance in Escrow account does not meet the definition of an asset of
the Company and therefore an adjustment has been made to de-recognize the asset
and related liability to the tune of the amounts available in the Escrow
account”
Kwa tafsiri yake ni kuwa: “Hivyo basi,
fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni
mali ya kampuni (TANESCO), hivyo marekebisho yamefanywa ili kutotambua mali na
madeni yanayohusu fedha hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo kwenye akaunti ya
Escrow.”
Kutokana na maelezo haya ni dhahiri kwamba
fedha zilizokuwa kwenye Escrow, siyo za TANESCO na hazikupaswa kuingizwa kwenye
vitabu vya TANESCO kama mali yake.
Chimbuko
la Sakata
Wazee
Wangu;
Chimbuko la kadhia yote hii Bungeni na kwenye
jamii ni uamuzi wa tarehe 5 Septemba, 2013 wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kuitambua
PAP kuwa mmiliki halali wa IPTL na kuagiza Mfilisi akabidhi shughuli zote za IPTL
kwa PAP. Katika utekelezaji wa uamuzi
huo wa Mahakama Kuu, ukazuka mjadala
mkali kuhusu fedha zilizomo kwenye akaunti ya ESCROW kukabidhiwa kwa PAP. Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya
Serikali miongoni mwa viongozi na watendaji wa Wizara na Taasisi zinazohusika
moja kwa moja na akaunti hiyo. Hizi ni
Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO na Benki Kuu. Viongozi na Watendaji husika walikuwa
wanajiuliza na kuuliza kama walipe au wasilipe.
Walipotaka ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakaelekezwa
watekeleze uamuzi wa Mahakama Kuu. Alisema uko sawa na hauna matatizo. Halikadhalika, Benki Kuu walipoulizia kuhusu
kodi za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza kuwa hakuna kodi ya
kulipwa.
Kwa kuzingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, malipo yakafanyika kwa IPTL tena bila ya kodi kulipwa. Baada ya malipo kufanywa ndipo mjadala huo
ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka kuwa kadhia kubwa, iliyochukua sura
ya kashfa yenye dalili za rushwa na wizi.
Uamuzi
Unaotiliwa Shaka
Wazee
Wangu na Ndugu Wananchi;
Kwa jumla uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu akaunti
ya Escrow, ushauri wa Mwanasheria Mkuu kwa Serikali wa kuelekeza uamuzi huo utekelezwe
na viongozi wa Serikali kutekeleza ushauri huo, vimetiliwa shaka. Umeonekana kuwa haukuwa uamuzi sahihi na
kwamba umeitia hasara nchi. Isitoshe
uamuzi huo umeibua hisia za kuwepo harufu na vitendo vya rushwa. Wapo waliosema
si bure iko namna! Wapo waliotaja majina
na watu wanaodai wamepata mgao wa Escrow tena wengine wamechukua fedha kwa
viroba, sandarusi na rumbesa. Bahati
mbaya sana katika mjadala, ilijengeka dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili
lilianzishwa na Maafisa hao wa Serikali kwa nia ya kujinufaisha wao
binafsi. Ukweli ni kwamba uamuzi
ulifanywa na Mahakama Kuu na kwenye Serikali ilikuwa utekelezaji wa amri hiyo.
Wazee
Wangu;
Nilipokutana na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kupata maoni yake kuhusu kadhia hii, ameendelea kusema alichosema
Bungeni kuwa hakukosea katika ushauri wake na wala Mahakama haikufanya makosa. Hivyo basi, hakuona sababu ya kwenda
Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi wa Mahakama kuhusu fedha zilizokuwepo
kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta kukabidhiwa kampuni ya PAP mmiliki wa
IPTL. Vilevile haoni kama kuna hasara yo
yote ambayo nchi imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL na imelipwa
IPTL.
Akifafanua, alisema kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa
kwa ajili ya kutunza fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa
yanafanywa na TANESCO. Kabla ya mzozo
kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo na kuanzishwa kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta,
TANESCO ilikuwa inalipa tozo ya uwekezaji moja kwa moja kwa IPTL. Baada ya kutokea mzozo na akaunti kuanzishwa
mambo mawili hayakubadilika. Kwanza
kwamba IPTL haikuacha kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO. Na, pili, kwamba TANESCO haikuacha kulipa
madai hayo. Mdai na mdaiwa
hawakubadilika. Kuwepo kwa akaunti ya
Escrow hakubadili mwenye fedha zake.
Akaunti hiyo iliundwa kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu
kiwango cha tozo. Matumaini ni kwamba
kama kiwango kitapunguzwa, TANESCO inaweza kupata nafuu ya malipo.
Kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe
fedha za akaunti ya Escrow, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni uamuzi
sahihi na wala taifa halikupata hasara kwa sababu pesa zimelipwa IPTL na siyo
mtu mwingine. Isitoshe anaona uamuzi wa
Mahakama umeisaidia TANESCO kutua mzigo mkubwa iliyokuwa nao kwa miaka saba.
Kama mjuavyo, akaunti ya Escrow
ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya tozo ya uwekezaji ya IPTL. Ilianzishwa kwa matumaini kuwa TANESCO
watapata nafuu ya tozo ya uwekezaji. Lakini,
hapakuwahi kufanyika mazungumzo baina ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo na
wala suala hilo halijafikishwa ICSID.
Haikuweza kufanyika hivyo kwa sababu washauri wa kisheria wa TANESCO
hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai kuwa hawafanyi
hivyo kwa sababu hakuna sababu mpya zinazoweza kupatikana kuifanya ICSID
ibadili uamuzi wake wa 2001 kuhusu kiasi cha tozo na namna ya ukokotoaji wake.
Matokeo yake ni TANESCO kuwa na akaunti
ya Escrow ambayo mwisho wake haujulikani.
TANESCO inaendelea kudaiwa na IPTL tozo ya uwekezaji na kulazimika
kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti
ya akaunti ya Escrow wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG mpaka tarehe 20
Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa inadaiwa shilingi
bilioni 103.8 ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola za Marekani milioni 33. Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti
ya Tegeta Escrow unalipatia unafuu TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni na riba.
Kwa upande wa kodi za Serikali ambazo
hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji Werema alisema yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama mamlaka husika inaona zipo
kodi zinazostahili kulipwa izidai.
Hakuna kilichopotea kwa sababu anayedai, yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo,
IPTL.
Uamuzi
wa ICSID II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji
Wazee
Wangu;
Yalitolewa mawazo kuwa kama fedha za akaunti ya
Tegeta Escrow zingelipwa baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya
Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICSID II) kutoa uamuzi wake, TANESCO
ingepata nafuu ya kupungua kwa tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba kuna
mambo mawili ya msingi. Kwanza kwamba
Mahakama hiyo haikutoa viwango vipya vya tozo kama ilivyofanya mwaka 2001
kwenye ICSID–I. Haikubadili mwongozo wa
ukokotoaji wa tozo. Imesema madai
yanaweza kuzungumzwa na kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo TANESCO watambue
kwamba wanahisa waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa kununua mtambo na pia
walikopa madeni, na kwamba kiasi cha fedha walichowekeza kilitakiwa kiwe na
kiwango cha juu zaidi cha faida.
Jambo la pili ni kwamba, shauri hili la pili
la ICSIDI II halikuihusisha kampuni ya IPTL mwenye Mkataba wa Kuuza Umeme na
TANESCO na siyo Benki ya Standard Charterd.
IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji wa uamuzi wa shauri hilo hapa
nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa TANESCO kufanya mazungumzo kwa msingi wa
shauri hilo.
Kinga
Dhidi ya Madai
Wakati wa kufunga akaunti ya Escrow, upande wa
Serikali ulielezea hofu yake ya uwezekano wa siku za usoni mtu kudai tena
kulipwa fedha hizi hizi ilizolipwa PAP. Nimeambiwa
kuwa suala hilo haliwezi kutokea kwani limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia. PAP imetiliana sahihi na Serikali kwamba
iwapo kutatokea mdai yo yote PAP itawajibika kulipa.
Mashaka
ya Miliki ya PAP kwa IPTL
Ndugu
Wananchi;
Hofu nyingine kuhusu uwezekano wa
Serikali kupata hasara ni yale madai kuwa huenda miliki ya PAP kwa asilimia 70
za hisa za IPTL zilizokuwa za kampuni ya Mechmar Berhard ya Malaysia siyo
halali. Pale mwanzoni ilidaiwa kuwa kampuni
ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya Piper Link ya British Virgin
Islands ilikuwa chini ya mchakato wa ufilisi kule Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria mtu hawezi
kuuza hisa zake akiwa kwenye mazingira hayo.
Katika uchunguzi wa CAG alieleza kuwa amethibitisha kwamba madai hayo si
kweli, Mechmar walipouza hisa zao tarehe
9 Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye ufilisi. Iliingia kwenye mchakato wa ufilisi mwaka
2012.
Lakini kwa upande wa kampuni ya Piper
Link ya Uingereza inasemekana iliuza hisa hizo baada ya kuwa wamepokea amri ya
Mahakama ya Malkia ya BVI kuizuia isiuze hisa hizo. Je ni kweli?
Imefanyika hivyo? Kama ni kweli
je PAP waliponunua hisa hizo walijua kama kuna zuio au hapana? Kama walijua basi na wao ni sehemu ya njama za
kufanya udanganyifu. Kama hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza uchunguzi wa kina ufanyike kupata
ukweli. Natambua hivi sasa Mahakamani
zipo kesi zinazohoji uhalali wa PAP kumiliki asilimia 70 za hisa za Mechmar
Berhad. Uchunguzi wetu hautaingilia
mchakato huo lakini unaipa Serikali fursa nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu
suala hili lenye mjadala mkubwa. Jambo lingine muhimu ambalo limeleta
matatizo kwa Mahakama zetu nchini na BRELA ni uuzaji wa hisa za IPTL au kuwekwa
rehani hisa hizo bila ya uamuzi huo kusajiliwa BRELA na kwenye Mahakama
zetu. Sheria zetu ambazo ndizo za nchi ya Jumuiya ya
Madola kama ilivyo kwa Hong Kong, Malaysia, na BVI, inaitaka kampuni ya Piper
Link ya BVI iliponunua hisa za Mechmar katika IPTL kusajili BRELA ununuzi
huo. Hali kadhalika, inaitaka SCB ya Hong
Kong na kupata amri ya Mahakama kuzuia deni la Mechmar na kuwekwa dhamana ya
hisa za Mechmar katika IPTL. Piper Link isiuze
hisa 70 za Mechmar katika IPTL. Walitakiwa
wasajili na BRELA na Mahakama yetu.
Kutokufanya hivyo ndiko kunazua maneno mengi na mzozo kuhusu uuzaji wa
hisa hizo kwa PAP. Kwa SCB wanapata
usumbufu wa kudai madeni yao IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi utakaofanyika utapata ukweli wa
yote kwa uhakika.
Ndugu
Wananchi;
Taarifa niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza
nanyi ni kuwa katika Mahakama zetu
nchini, kuna mashauri yahusuyo miliki ya
PAP ya hisa 70 zilizokuwa za Mechmar katika IPTL na yapo mashauri yahusuyo PAP
kupewa fedha za akaunti ya Escrow. Zipo
pia nyingine za masuala mbalimbali, yakiwemo mashauri yaliyofunguliwa na PAP
dhidi ya watu, na makampuni binafsi na vyombo vya Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama zetu utatoa majibu
kwa masuala yote hayo.
Pamoja na hayo yatakayokuwa yanaendelea
Mahakamani, Serikali itaendelea kufanya uchunguzi wake na kuamua namna ya
kushughulikia taarifa zitakazopatikana ili nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu
kufanya hivyo.
Jambo lingine muhimu nataka uchunguzi
wa kina ufanyike ni kujua nani ni nani katika uuzaji na ununuzi wa hisa za
Mechmar. Hususan nataka tujue kwa ukweli
na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa bei gani.
Je, ni kweli gharama zinazosemwa ndizo
zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli huo ili
tujue kodi yetu ya ongezeko la mtaji (Capital
Gains Tax) inayostahili kulipwa Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani
kimelipwa na kipi hakijalipwa ili kidaiwe?
Tuhuma
za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa
Wazee
Wangu;
Kumekuwepo na tuhuma za vitendo vya rushwa
katika mchakato mzima wa kufunga akaunti ya Escrow na kukabidhi fedha hizo kwa
kampuni ya PAP. Halikadhalika,
kumekuwepo na hisia hizo hizo kwa upande wa jinsi kampuni ya VIP Engineering
and Marketing ilivyotumia pesa zake zilizoko kwenye Benki ya Mkombozi. Yamesemwa mengi sana na mmeyasikia na
kuyasoma.
Rushwa ni kosa la kijinai ambalo kwa
Serikali yetu ni kosa ambalo ni vigumu kulivumilia wala kulifumbia macho. Mara
baada ya kupata fununu za uwezekano wa vitendo hivyo kufuatia taarifa ya awali
ya CAG ya kwenda kukagua miamala, niliagiza taarifa husika zifikishwe kwenye Taasisi
ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa uchunguzi zaidi. Naambiwa taarifa hizo zimefika na kazi ya
uchunguzi inaendelea. Tayari watu kadhaa
wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa.
Wakati nawasihi wananchi kuvuta subira ili tuwape nafasi PCCB wakamilishe
kwa ufanisi wa hali ya juu kazi yao waliyokwishaianza, nawaomba PCCB waongeze
kasi ya uchunguzi. Napenda kufafanua
kwamba kwa upande wa miamala iliyotoka katika akaunti ya kampuni ya VIP
Engineering and Marketing ya Ndugu James Rugemalila, Serikali inashughulika na
watumishi wa umma kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma, maana
suala lao ni la kimaadili. Hatuwahoji
wasiokuwa watumishi wa umma.
Maazimio
ya Bunge
Ndugu
Viongozi;
Wazee
Wangu;
Ndugu
Wananchi;
Niliona nianze kwa kutoa maelezo hayo
ya utangulizi kabla ya kuyazungumzia maazimio ya Bunge. Serikali imepokea maazimio hayo ya Bunge na
kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji wake.
Nawapongeza Wabunge wetu kwa moyo waliouonesha wa kuchukia maovu na
kutaka yashughulikiwe ipasavyo. Napenda
kuwahakikishia kuwa niko pamoja nao. Nampongeza
Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika na
Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu kwa uongozi wao mahiri. Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini chini ya
uongozi wao mambo yameisha salama na tumepata maazimio nane yanayozungumzika na kutekelezeka. Nawashukuru na kuwapongeza sana Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uongozi wa Mheshimiwa
Zitto Kabwe na Mheshimiwa Deo
Filikunjombe na pia Wajumbe waliounda Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia mwafaka
wa mapendekezo haya 8 ambayo yaliazimiwa na Bunge.
Mwisho lakini si ya mwisho kwa umuhimu,
nawapongeza Wabunge wote kwa michango yao mizuri. Jambo lililonifurahisha sana ni ushirikiano
wa Wabunge wa kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili muhimu,. Hivi ndivyo inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze mshangao wangu
niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya maamuzi yale ni yao wao na
wenzao hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali ina Wajumbe 19
wa CCM na wa Upinzani 5. Bunge lina
Wabunge wa CCM asilimia 74 na wa
upinzani asilimia 26. Hivi kama ni
yao wao pekee na wa upande wa CCM wangepinga yangekuwa? Yasingefika po pote, yangefia kwenye
Kamati. Huku ni kutafuta umaarufu kwa
mgongo wa wengine. Na, Wabunge wengi wa
CCM na nyie semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote.
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu
wa dhamira ya kutekeleza yale maazimio yanayoangukia katika dhamana yetu. Napenda kuainisha mtazamo na mwelekeo wa
Serikali katika utekelezaji wa maazimio hayo manane kama ifuatavyo:-
Azimio
la kwanza:
Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL
na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Pendekezo tumelipokea, ni jambo linalowezekana
kufanya. Hata hivyo, tunapopima ujumbe tunaoupeleka
kwa jumuiya ya wawekezaji tunachelea kuwa inaweza kuleta hofu na kuwatisha
wawekezaji waliopo na wajao. Nalisema hivyo kwa sababu sisi tuna historia
ya kutaifisha mali za kamapuni binafsi. Hofu
hiyo bado ipo. Tukichukua mitambo hii
tunaweza kurudisha hofu za kurudi tulikokuwa na kukimbiza mitaji tunayohitaji
kwa uchumi kukua na nchi kupata maendeleo.
Nashauri tuendelee kuyapatia ufumbuzi matatizo ya IPTL kila
tunapoyabaini. Aidha, Mahakama imetusaidia sana kwa kuamuru
mitambo ya IPTL ibadilishwe ili itumie gesi asilia na kutoza bei ya umeme
isiyozidi senti nane za Marekani. Tuyafuatiliye
haya kwanza.
Azimio
la Pili:
Azimio hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa Mikataba linasomeka
ifuatavyo: “Bunge limeazimia kwamba
Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekavyo na kwa vyovyote
vile kabla ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti.
Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya
umeme”.
Azimio hili tumelipokea na tunaangalia namna
bora ya kulitekeleza ili kuweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kuitikia kilio cha muda mrefu kuhusu
uwazi katika mikataba ambayo Serikali inaingia na wawekezaji; na pili
kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki ya wawekezaji hao dhidi ya
washindani wao inazingatiwa. Serikali na
Bunge tutakaa chini hivi punde kutafuta namna bora ya kisheria na tutafanya
hivyo kwa kujifunza pia kutokana na uzoefu wa nchi ambazo zina utaratibu wa aina
hii.
Azimio
la Tatu:
Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo
vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahili kwa mujibu wa
sheria za nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye taarifa maalum ya Kamati
husika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya ESCROW,
na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea
kuhusu kuhusika kwao katika vitendo hivyo vya jinai”
Vyombo
husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na inaendelea. Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa
kwa mujibu wa sheria.
Azimio
la nne:
Linasomeka, “Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa zao wenyeviti wa Kamati za
Bunge waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP Engineering kabla ya kikao kijacho
cha Bunge”
Azimio hilo liko chini ya mamlaka ya
Bunge lenyewe. Nawaachia wao waamue.
Azimio
la Tano:
Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya
Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya
Tanzania”
Azimio hili nimelipokea, tumelijadili hata
hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia
masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama
hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya
kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inaporidhika
kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa
Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa.
Azimio
la Sita:
“Bunge linaazimia kwamba mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi
kuitaja Stanbic Bank Ltd. na benki yeyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi
wa mamlaka ya uchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa
katika akaunti ya ESCROW kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha
haramu (Institutions of money laundering concerns).
Pendekezo la Bunge ni zuri kwamba
mamlaka husika na udhibiti wa vitendo vya utakatishaji fedha vifanye uchunguzi kwa
mujibu wa Sheria. Serikali imelipokea na
mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units kulishughulikia. Naamini wameshaaza, tuwape muda watimize
wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Azimio
la Saba:
“Bunge liliazimia kwamba Serikali iandae, na kuwasilisha Muswada wa
Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la kuanzishwa Taasisi
mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa,
ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Kazi ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU
inaendelea. Tayari Sheria mbalimbali
zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya
mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Fedha Haramu ya mwaka 1991 ambazo
zote zinaweka utaratibu wa kushughulikia vitendo vya rushwa. Tutaendelea kuziboresha sheria hizo kwa kadri
itakavyohitajika. Kazi iliyopo mbele
yetu ni kuimarisha usimamizi wa sheria hizo.
Jambo hilo nalo litazingatiwa katika maboresho hayo. Ni dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza
kupambana na kushinda vita dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari kulifanyia kazi
pendekezo lolote linaloimarisha dhamira yetu hii njema.
Azimio
la nane:
“Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi na
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO
wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Azimio hili ndilo Azimio ambalo
limevuta hisia za watu wengi, na pengine ndilo ambalo utekelezaji wake
unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji wake
umeanza. Kwanza, ni kuhusu Bodi ya
TANESCO, tumeanza mchakato wa kuunda
Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza muda wake.
Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma anatawaliwa na Sheria
na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma
zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering
and Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule anayoimiliki na
kuiendesha. Mwenyewe ameeleza wazi
kupitia vyombo vya habari. Pamoja na hayo yapo mambo ya msingi kimaadili ambayo
hayakuzingatiwa, hivyo tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu Prof. Muhongo nimemuweka kiporo, kuna
uchunguzi niliagiza ufanywe na vyombo vyetu bado nasubiri taarifa hiyo ili
nifanye uamuzi ndani ya siku chache zijazo.
Hitimisho
Wazee
Wangu;
Nawashukuruni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment