Watu wasiofahamika, usiku wa kuamkia jana wameandika maneno
kwenye kuta ikiwamo ukuta wa Kampuni ya Bakhressa katika maeneo ya Tazara
wakidhihaki Katiba Inayopendezwa sanjari na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema inafuatilia
kubaini watu wanaoandika maneno ya uchochezi kwenye kuta na kwamba
wakigundulika watashitakiwa kwa uchochezi na uvunjifu wa amani.
Miongoni mwa maandishi kwenye kuta hizo, yalitaka ipigwe
kura ya hapana kwa Katiba Inayopendekezwa na kwamba ni mbovu. Mengine
yalimshutumu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.
Kamanda wa Polisi katika hiyo Maalumu, Suleiman Kova alisema
wanaendelea kuwatafuta ili kuweza kuwabaini na kuwafikisha mahakamani.
Alisisitiza jamii kutumia njia mwafaka ya kufikisha mawazo yao.
Alisema kwa kutoa maoni kwenye kuta hayana thamani, kwani
hakuna atakayefanyia kazi lakini kwa kufuata taratibu yataheshimiwa.
Kutokana na maandishi hayo yaliyokutwa jana asubuhi,
wafanyakazi wa kampuni hiyo ya Bakhressa walilazimika kuyafuta kwa kupaka rangi
upya kwenye ukuta huo.
Mmoja wa vijana waliokuwa wakifuta maandishi hayo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan, alisema baada ya uongozi kupata
taarifa ya kuwepo maandishi hayo waliwataka kufuta na kupaka rangi upya.
Hivi karibuni, iliripotiwa kwamba mkoani Dodoma, maandishi
kama hayo yalikutwa katika ukuta wa ofisi za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
No comments:
Post a Comment