UDA YAZINDUA WIKI YA 'SAFIRI SALAMA'


Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limezindua wiki ya huduma kwa wateja yenye kauli mbiu ya ‘Safiri Salama’ ambayo mbali na mambo mengine lengo lake ni kuwawezesha watumiaji wa usafiri huo kutoa maoni yao juu ya huduma zinazotolewa na shirika hilo.
Katika taarifa ya shirika iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, Msemaji wake, George Maziku alisema, huduma hiyo inayotarajiwa kumalizika Jumamosi wiki hii.
Itahusisha wafanyakazi wao kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwamo ndani ya mabasi ya shirika hilo kwa lengo la kufahamu uhusiano kati ya makondakta, madereva na wasafiri wa UDA.
Alisema lengo jingine ni kuwawezesha  wateja wanaotumia mabasi ya kampuni hiyo kufahamu huduma zao, zikiwemo huduma za kukodi mabasi na kutangaza biashara zao kupitia mabasi hayo.
Alisema hiyo itatoa fursa ya wateja kutoa mapendekezo ya uboreshaji wa  huduma zake na sekta nzima ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam kwa ujumla.
Aliwataka wateja kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kuongea bayana bila woga wowote upungufu wa huduma zao, hususan tabia za madereva pamoja na makondakta kwa lengo la kusaidia kuboresha zaidi huduma za shirika hilo.
Maziku alisema kuwa wiki hii ya huduma kwa wateja, itatoa taswira halisi ya kufahamu wateja wanapenda na wanataka nini kiboreshwe katika huduma za shirika hilo, na pia itatoa picha ya kufahamu kuwa wateja wanaridhika au hawaridhiki na huduma za shirika hilo.
Wiki ya Huduma kwa Wateja ni wiki ya kimataifa ambayo huadhimishwa kuanzia Oktoba 6 mpaka 10, kila mwaka ambayo mashirika na makampuni mbalimbali huadhimisha kwa kuwatembelea wateja wao kwa lengo la kusikia maoni yao.

No comments: