WANAFUNZI 100 WATUMIA CHUMBA KIMOJA CHA DARASA


Wanafunzi 100 katika shule ya msingi ya Elerai ya jijini Arusha wanalazimika kutumia darasa moja kwa ajili ya kujisomea kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa unaoikabili shule hiyo. 
Hayo yalisemwa jana jijini hapa  kwenye mahafali ya darasa la saba shuleni hapo na mkuu wa shule hiyo, Raymond Mushi. 
Alisema shule yake inakabiliwa na uhaba wa vyumba 16 vya madarasa, hali ambayo imefanya wanafunzi zaidi ya 100 kujibana katika darasa moja. 
Mushi alisisitiza ya kuwa pamoja na kero hiyo, lakini jumla ya wanafunzi 203 wa darasa la saba shuleni hapo wanatarajiwa kufanya mtihani wao wa kuhitimu elimu ya msingi mwezi huu. 
Kutokana na hali hiyo mmoja wa wakazi wa kata ya Elerai inayozunguka eneo la shule hiyo, Kake Dhariwal ameamua kujitolea msaada wa zaidi ya Sh milioni 58 kwa lengo la kugharamia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ili kupunguza kero hiyo. 
Dhariwal, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya AVCO  Investment Limited ya jijini Arusha mbali na kutoa msaada huo pia alijitolea kuunganisha maji, umeme pamoja na kutoa msaada wa matofali 200 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta wa shule hiyo.

No comments: