Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Antony Mahwata jana alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Njombe akikabiliwa na mashitaka ya kutishia kumuua kwa maneno Mbunge wa zamani wa Jimbo la Njombe Magharibi, Yono Kevela.
Mahwata ameunganishwa na Evaristo Makurumbi katika kesi hiyo namba 107/2014 ambapo mlalamikaji ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka Atupakisye Mwakasitu mbele ya Hakimu Samwel Obasi kuwa Mahwata anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kutishia kuua kwa maneno na uvunjifu wa amani kwa kuleta fujo kwenye mchezo wa mpira, huku Makurumbi akikabiliwa na kosa la kuleta fujo pekee.
Mwendesha Mashitaka Mwakasitu alisema washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 5, 2013, katika Kijiji cha Igwachanya wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa wanadaiwa kumtishia kumuua kwa maneno Yono na kuleta fujo kwenye mchezo wa mpira wa miguu uliofanyika katika Kijiji cha Igwachanya, wakati timu ya Yanga Veterans ya Dar es Salaam walipocheza na timu ya soka ya Igwachanya.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba washitakiwa walileta fujo kwa kuweka magari yenye namba T.749 AYU aina ya Toyota Rav 4 mali ya Mahwata na T 973 aina ya Toyota Noah mali ya Makurumbi katika magoli yote mawili ya kiwanja cha mpira cha Igwachanya kwa lengo la kuvuruga mchezo huo kuchezwa.
Washitakiwa walikana mashitaka yanayowakabili. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Septemba 9, mwaka huu katika mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment