WAJUMBE WATAKA MSAJILI AWEZESHWE KUFUTA VYAMA KOROFI


Baadhi ya Kamati za Bunge Maalumu la Katiba zimependekeza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini apewe nguvu na Katiba awe na mamlaka ya kufuta chama chochote cha siasa kinachokiuka masharti ya kusajiliwa, ikiwemo kuleta uchochezi kama njia ya kufikia malengo yake ya kisiasa. 
Ibara ya 197 ya Katiba inayopendekezwa inaelezea kazi mbalimbali za msajili, lakini wajumbe wa Bunge sasa wanataka pia chama ambacho hakizingatii usawa wa jinsia katika uongozi wake, au kinaonekana kukuza na kupigania maslahi ya kundi lolote la dini, la kikabila, pahala watu watokeapo, rangi au jinsi. 
Miongoni mwa masharti hayo ni kama kitakuwa na wanachama upande mmoja wa Jamhuri, kuwa chama cha kikabila, kikanda na chama ambacho kitachochea vurugu kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa. 
Rasimu ya Katiba inaeleza wajibu wa msajili wa vyama itakuwa ni kusimamia na kuratibu uandikishaji  na shughuli za vyama vya siasa, kutayarisha na kuchapisha taarifa za kila mwaka kuhusu ripoti za ukaguzi wa fedha na kusimamia fedha za vyama vya siasa. 
Pia kamati hiyo inapendekeza kuwe na naibu msajili wa vyama vya siasa atakayeteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na tume ya utumishi wa umma, ambaye atakuwa msaidizi mkuu wa msajili wa vyama vya siasa. 
Kamati namba nane katika eneo hilo, ilipendekeza uteuzi wa msajili na naibu msajili wa vyama vya siasa utafanywa kwa misingi kwamba endapo msajii wa vyama vya siasa atateuliwa  kutoka Tanzania Bara, naibu msajili atateuliwa kutoka Zanzibar. Wote hao wanatakiwa wawe raia wa kuzaliwa na wazazi wao pia wawe raia wa kuzaliwa. 
Kamati namba nane imependekeza msajili wa vyama vya siasa aongezewe majukumu ya kutayarisha na kuchapisha taarifa za kila mwaka kuhusu ripoti ya ukaguzi wa fedha kwa kila chama cha siasa kinachopata ruzuku kutoka serikalini kama ilivyo katika sheria za nchi, kutatua migogoro ya vyama vya siasa, kufanya ukaguzi wa uhai wa vyama vya siasa na kuelimisha jamii. 
Kuhusu tume huru ya uchaguzi, Kamati namba 12 katika pendekezo lake imetaka wajumbe wa tume huru ya uchaguzi wasithibitishwe na Bunge kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya mabadiliko ya katiba. 
Katika mapendekezo hayo kamati hiyo inadai kuwa haja ya majina yaliyopendekezwa na Rais kuthibitishwa na Bunge, badala yake wanataka ibara hiyo isomeke kuwa rais  atateua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa tume huru ya uchaguzi kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa na kamati ya uteuzi. 
Kamati hiyo pia imependekeza kufutwa kifungu kinachowapa fursa asasi za kiraia na zisizo za kiserikali kuwa zinaweza kupendekeza majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa tume huru ya uchaguzi. 
Kamati hiyo pia imependekeza tume huru ya uchaguzi iongezwe kazi kwa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, wabunge na Rais na kutangaza matokeo ya chaguzi hizo. 
Rasimu ya katiba inapendekeza tume hiyo kusimamia uchaguzi wa Rais na Wabunge na kura ya maoni, uandikishaji wa wapiga kura, kugawa na kutangaza majimbo ya uchaguzi ya wabunge.

No comments: