UAMUZI KUPINGA BUNGE LA KATIBA KUTOLEWA SEPTEMBA 15


Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 15, mwaka huu, kutoa uamuzi wa pingamizi la awali lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), dhidi ya ombi la kusimamishwa kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mkoani Dodoma. 
Jopo la majaji watatu  likiongozwa na Jaji Augustine Mwarija, wengine ni Dk Fauz Twaib na Aloysis Mujulizi, lilisema hayo jana, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika kesi hiyo. 
Katika ombi hilo Mwandishi wa Habari Said Kubenea kupitia Wakili wake Peter Kibatala anaiomba mahakama hiyo itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo,  wakati wakisubiri uamuzi kuhusu tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge la Katiba. 
Hata hivyo, AG aliwasilisha pingamizi akiwa na hoja tatu akidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusimamisha Bunge hilo kwa kuwa ni halali Kikatiba na mchakato wake ulifanyika chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. 
Alidai ombi hilo ni batili na halina msingi kisheria na kuongeza kuwa Kubenea anaomba Bunge lisimamishwe kwa sababu ya kusubiri tafsiri ya kifungu kimoja cha sheria, pia Bunge hilo halijafanya uamuzi ambao unaweza kufikishwa mahakamani kulalamikiwa. 
Alidai bunge hilo bado lipo katika hatua ya kutunga sheria, hivyo anaomba ombi hilo litupiliwe mbali kwa sababu ni batili. 
Mawakili Wakuu wa Serikali Wakili George Malata na Edson Mweyunge walidai kifungu kilichotumika kuleta ombi hayo si sahihi, pia hati ya kiapo inayounga mkono ombi hilo ina mapungufu ya kisheria. 
Wakili wa Kubenea, Kibatala aliomba mahakama itupilie mbali pingamizi hili kwa kuwa halina msingi kisheria kwa kuwa ombi lao limewasilishwa kwa mujibu wa sheria. 
Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri ya mamlaka ya bunge hilo chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba Namba 83 ya mwaka 2011. 
Aidha anaiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa ombi la tafsiri hiyo. Amewasilisha ombi hilo chini ya hati ya dharura. 
Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria na pia itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha malengo ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.

No comments: