SASA NI JESHI DOGO, LA KISASA NA MASLAHI BORA ZAIDI


Serikali iko katika mkakati madhubuti wa kuliboresha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kuwa na jeshi dogo lenye maslahi bora, silaha za kisasa zinazokwenda na wakati na kuwa na vyombo vya usafiri vya barabarani, angani na majini. 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Jakaya Kikwete wakati akifunga hitimisho la zoezi la medani la maadhimisho ya mafunzo wa JWTZ ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo katika kijiji cha Nangalulusu wilayani Monduli Mkoani Arusha. 
Alisema JWTZ kwa kipindi cha nusu karne imepata mafanikio makubwa sana tofauti na ilivyoanzishwa Septemba mosi mwaka 1964 na kutokana na hali hiyo serikali iko katika mkakati madhubuti wa kuliboresha jeshi hilo kuwa jeshi dogo na imara na lenye maslahi mazuri, silaha za kisasa, vyombo vya usafiri vya kisasa vya angani, barabarani na majini na kuwa na wanajeshi wasomi na weledi. 
Rais Kikwete alisema kufanya hivyo ni kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii katika kulinda mipaka ya nchi na kutoa huduma za elimu, afya na kujitoa katika kusaidia majanga mbalimbali yanayotokea kote nchini. 
Alisema  JWTZ tangu kuanzishwa kwake imeilinda  misingi imara na madhubuti ya jeshi iliyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni pamoja na jeshi lenye utii na nidhamu na jeshi lenye kulinda uhuru na mipaka yake. 
Rais alisema JWTZ imeweka historia katika Afrika kwa kupigana vita mwaka 1978 na Uganda na kulifuta kabisa jeshi la nchi hiyo na kushiriki kikamilifu katika ukombozi wa baadhi ya nchi barani Afrika, hali ambayo inapaswa kupongezwa kwa kufanya kazi nzuri na ya kujivunia. 
Alisema kwa sasa kuna mabadiliko mbalimbali duniani na matishio mapya hivyo jeshi linapaswa kushiriki kikamilifu, ikiwa ni njia mojawapo ya kutimiza majukumu yake. 
“Nikienda katika nchi mbalimbali marais wenzangu wananisifu kwa kuwa na jeshi imara lenye nidhamu na  kufanya kazi yake kwa uhakika na weledi mkubwa hivyo ni lazima niwapongeze kwa hilo,” alisema. 
Rais alisema kabla ya kuondoka madarakani atahakikisha anajenga hospitali kubwa ya kisasa ya jeshi la wananchi, kwa ajili ya kutibu magonjwa maalumu ya wanajeshi yanayowakuta katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku, ikiwa na kukamilisha ujenzi wa nyumba za wanajeshi 3,636 ambako kwa sasa ujenzi wa nyumba 10,000 umeshakamilika.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amemwomba Rais kuhakikisha fedha zinazoombwa na wizara yake katika bajeti zinatoka kwa wakati ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa na wizara hiyo. 
Mwinyi alisema jitihada za kulipatia jeshi zana za kisasa ni kielelezo cha uthibitisho jinsi askari wanavyohitaji kulinda nchi kwa kuwa na silaha za kisasa zikiwemo ndege za kivita, mizinga na vifaru. 
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyaje alisema madhumuni ya mazoezi hayo kuwaweka tayari wanajeshi wakati wowote katika majukumu yao ya ulinzi wa nchi na nchi za bara la Afrika. 
Pia ni wajibu wa jeshi hilo kulinda mipaka ya nchi, wananchi na mali zao na kufanya shughuli za ndani ya nchi pindi wanapohitajika.

No comments: