TANZANIA YA NANE DUNIANI KWA MATUKIO YA KUJIUA



Wakati imethibitishwa kwamba katika kila sekunde 40 mtu mmoja duniani huamua kukatisha maisha yake kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika, Tanzania imeelezwa kuwa ya nane katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa watu wake kujiua.
Ingawa Jeshi la Polisi nchini lilipotakiwa kuzungumzia suala hilo lilionekana kuchukua mlolongo mrefu, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), umesema tabia ya watu kuficha takwimu na kufuatilia matukio ya vifo inachelewesha uchukuaji hatua wa kudhibiti tabia hiyo ya kujiua.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bukumbi juzi alipotakiwa kuthibitisha kwa takwimu kuhusiana na utafiti huo wa WHO, sababu za kujiua na hata mikoa inayoongoza kwa matukio ya aina hiyo nchini, alitaka mwandishi wa habari hizi kumtumia maswali ili yafanyiwe kazi kuanzia wiki ijayo.
Utafiti uliofanywa na WHO na kutolewa kama Taarifa na Umoja wa Mataifa juzi, unaonesha kwamba tatizo la kujiua halitiliwi maanani wala kujadiliwa kutokana na kunyanyapaliwa na kuwepo kwa imani potofu zinazohusishwa na vifo hivyo.
Katika utafiti uliotolewa wiki tatu baada ya mmoja wa wakali wa Hollywood Robin Williams kujiua, pia waandishi wa habari wameonywa dhidi ya kuelezea kinagaubaga vifo hivyo kutokana na hatari ya watu wengine kunakili tabia na maamuzi hayo kwa jinsi yalivyoelezwa na vyombo vya habari.
WHO, ambayo imesema kwamba kujitwalia maisha binafsi ni tatizo kubwa la kiafya duniani kwa sasa linalohitaji hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yake imetoa taarifa hiyo baada ya kufanya uchunguzi katika nchi 172 duniani.
Imesema katika mwaka 2012 nchi zenye kipato kikubwa ziliongoza kwa mauaji ya aina hiyo ikiwa na vifo asilimia 12.7 kwa kila watu 100,000 huku nchi za kipato cha chini na kati zikiwa ni asilimia 11.2 kwa kila watu 100,000.
Lakini kutokana na nchi za kipato cha chini na kati kuwa na wingi wa watu, wao ndio waliochukua nafasi kubwa ya vifo hivyo, kwani robo tatu ya matukio kwa wastani yapo katika nchi hizo.
Hata hivyo, nchi za Kusini Mashariki mwa Asia  zikiwemo Korea Kaskazini, India, Indonesia na Nepal  ndizo zimefanya theluthi moja ya waliojiua duniani.
Vifo vya  kujiua katika nchi tajiri vinaelezwa kuwa wastani wa robo ya vifo vinavyotokea duniani kote vya aina hiyo.
Aidha utafiti huo umeonesha kwamba njia kubwa inayotumika karibu duniani kote ni kutumia sumu za mashambani, kujinyonga, kujipiga risasi na kuruka kutoka katika majengo marefu tabia ambayo ipo zaidi katika nchi za Asia, hasa maeneo ya miji.
"Kila kifo cha kujiua huleta huzuni. Inakadiriwa kwamba watu zaidi ya laki nane hufa kwa kujiua. Lakini pia wapo watu wengi wanaojaribu kujiua kwa namna tofauti," alisema Mtendaji wa WHO, Dk Margaret Chan akihitimisha miaka kumi ya utafiti wa tatizo hilo.
Alisema kwamba athari inayopatikana kwa familia, marafiki na jamii ni kubwa hata kama watu hao wanakuwa wamejiua wenyewe.
WHO wamesema takwimu za watu wanaojiua hazipo sawa kutokana na nchi nyingi kutokuwa na tabia ya kuweka takwimu hizo.
Kutokana na upungufu huo, walilazimika kufanya kazi ya ziada ili kuweza kupata wastani wa watu wanaojiua nchi kwa nchi.
Wastani wa dunia wa watu kujiua upo kwa watu 11.4 kwa kila watu 100,000 huku wanaume kama wanawake kwa idadi sawa wakijaribu kujiua.
Nchi ambazo zinaongoza kwa vifo vya kujiua ni Guyana (asilimia 44.2 kwa kila watu 100,000), ikifuatiwa na Korea Kaskazini na Korea Kusini (asilimia 38.5 na 28.9 kwa kila 100,000).
Nchi nyingine ni Sri Lanka (28.8), Lithuania (28.2), Suriname (27.8), Msumbiji (27.4), Nepal na Tanzania (24.9 kila mmoja), Burundi (23.1), India (21.1) na Afrika Kusini (19.8).
Nchi nyingine ni za Russia na Uganda (zote zikiwa na wastani wa 19.5), Hungary (19.1), Japan (18.5) na Belarus (18.3).
Katika nchi zenye kipato kikubwa matatizo ya afya ya akili kama msongo wa mawazo umeelezwa kusababisha asilimia 90 ya vifo vya kujiua ukilinganisha na asilimia 60 katika nchi za Asia kama China na India, WHO imesema.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kwamba ni lengo ifikapo mwaka 2020 kuhakikisha kwamba wanapunguza wastani wa kujiua kwa asilimia 10.
Hata hivyo, utafiti umeonesha kuna changamoto kubwa kutokana na vifo hivyo kutokea katika makundi ambayo yanaonekana kutengwa, wengi wao wakiwa masikini, wenye matatizo mbalimbali na wanaoishi katika hali ya kutothaminiwa au kukubalika katika jamii.
Utafiti umeonesha kwamba nchi zenye pato dogo ambazo zinahangaika kuwatimizia wananchi wake mahitaji muhimu yakiwemo ya afya, kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza wana wakati mgumu wa kutambua na kuwasaidia watu wanaotaka kujiua.
Dk Chan anaamini kwamba vifo vya aina hii (vya kujiua) vinaweza kuzuiwa.
Ametaka nchi mbalimbali kuendelea na kazi ya kuzuia vifo vya kujiua na hata nchi ambazo hazina watu wanaojiua zifanye juhudi ya kuhakikisha kwamba zinazuia kutokea kwa vifo hivyo kwa kuwa wazi kujadiliana na kuweka katika ajenda.
Hata hivyo wataalamu wamekuwa wakishutumu vyombo vya habari na vile vya kijamii kwa kuelezea jamii kinagaubaga vifo hivyo hali ambayo inaweza kutumiwa na watu wengine kujiua.
"Kuna kutowajibika kwa vyombo vya habari katika suala hili, wanaandika tu, wanakuwa chachu, habari zao huchochea vifo zaidi," inasema taarifa hiyo  huku ikisisitiza kwamba namna zinavyoandikwa ni kama vile kuremba aina hiyo ya kufa na kuiona kwamba ni hali ya kawaida.
Akizungumzia utafiti huo katika mahojiano na gazeti hili, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema ni jukumu la wizara yake kuhakikisha amani katika familia inadumishwa.

Alisema kujiua ni kosa la jinai na pia ni dhambi, hivyo wizara yake inahamasisha upendo ndani ya familia kuwepo na mazungumzo ili kuepuka matatizo yanayosababisha watu kujiua.

“Jamii itambue ni vizuri kuongea ndani ya familia tangu watu wakiwa wadogo ili inapoonekana dalili ya tatizo lipatiwe ufumbuzi na sisi kama wizara, kazi yetu ni kuhamasisha familia kuishi kwa upendo na mawasiliano ya mara kwa mara,” alisema Waziri Simba.

No comments: