Rais Jakaya Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia
vifo vya watu 39 vilivyotokea katika ajali ya barabarani wilayani Butiama, Mkoa
wa Mara, ambako pia watu 75 wameumia, baadhi yao vibaya.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo iliyotokea jana asubuhi, Rais Kikwete
ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Arusha, amemtumia salamu
za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, akielezea huzuni na masikitiko yake.
“Nakuomba uwafikishie wafiwa wote
pole zangu nyingi sana, ukiwajulisha kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu
cha maombolezo. Aidha, napenda uwajulishe kuwa naungana nao kumwomba Mwenyezi
Mungu aziweke pema roho za marehemu.”
Kufikia jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Phillip Kalinji alisema hakuna
watu zaidi waliopoteza maisha. Aidha, alisema wote waliokufa, isipokuwa wawili
tu, miili yao imetambuliwa na ndugu zao.
Hata
hivyo, alisema hakuwa katika nafasi nzuri ya kuwataja marehemu na majeruhi wa
ajali iliyohusisha magari matatu, yakiwemo mabasi yaliyogongana uso kwa uso na
gari dogo aina ya Nissan Teranno lililogongwa na kutumbukia mtoni.
Mabasi
yaliyogongana juzi majira ya saa 5:30 asubuhi ni Scania lenye namba za usajili
T 736 AWJ mali ya Kampuni ya Mwanza Coach lililokuwa linatokea Musoma kwenda
Mwanza na lingine aina ya Zoutong, lenye namba za usajili T 677 CYC mali ya
Kampuni ya J4 Express lililokuwa linatokea Mwanza kwenda Musoma. Gari dogo
lililogongwa aina ya Nissan Terrano lina namba za usajili T 332 AKK.
Mwandishi alifanikiwa
kuwafahamu waliokufa kuwa ni daktari wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, Dk Anatoria
Ntangeki na Sayi Hassan aliyekuwa Mhandishi wa Mradi wa Umwagiliaji mkoani
Mara.
No comments:
Post a Comment