MCHUNGAJI AFARIKI NA MIAKA 114, AACHA MJANE WA MIAKA 30


Mchungaji Samuel Sadela (114), wa Kanisa la Gospel Apostolic aliyehubiri kwa miaka 82 amefariki dunia na kuacha mjane mwenye umri wa miaka 30 aitwaye Christina aliyemuoa miaka saba iliyopita. 
Mchungaji Sadela alioa mke wa tatu, Christina mwaka 2007, baada ya kufiwa na mke wake wa pili mwaka 1965 ambaye alizaa naye watoto wanne na wawili kati ya hao walifariki na mkewe huyo alifariki mwaka 2001. 
Awali, Ofisa Mwandamizi mmoja wa juu wa kanisa hilo lililopo kwenye Wilaya ya Gdagada, Lagos aliviambia vyombo vya habari vya kimataifa kuwa, mchungaji huyo alifariki dunia Jumapili iliyopita baada ya kuugua kidogo maradhi yanayohusishwa na uzee kutokana na umri wake. 
“Papa (Sedela), amekufa baada ya kuugua muda mfupi, tunamkumbuka mchungaji wetu na mlezi wa kanisa enzi za utumishi wake,” alisema Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe. 
Mchungaji Sadela, alisifika sana kwa huduma yake na kusafiri maeneo mengi ndani na nje ya Nigeria akihubiri neno la Mungu na nchi alizowahi kuhubiri ni kama vile Marekani na Uingereza na kwamba alikuwa akisisitiza kuwa amezaliwa mwezi Agosti,  mwaka 1900, ingawa hakuna nyaraka zinazothibitisha hilo. 
Taarifa zinasema, ikiwa ni kweli mchungaji huyo amezaliwa mwaka huo, basi angekuwa ndiye mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani kwa mujibu wa Kitabu cha Maajabu ya Rekodi za Dunia. 
Mamia ya waombolezaji wa kanisa hilo walionesha huzuni zao huku wakijipanga kwenye mstari mrefu kwenda kusaini kitabu cha maombolezo kilichowekwa kwenye viwanja vya kanisa hilo. 
Kabla ya kuoa mke wake wa pili, Papa Sedela alikuwa na mke wa kwanza ambaye alizaa naye watoto saba, ambao pia wote walifariki wakiwa wadogo na mkewe huyo akafa baada ya miaka 21 ya ndoa. 
Katika enzi za uhai wake alikuwa akisema anajisikia kijana na mwaka jana alisherehekea siku ya kuzaliwa kwake akiadhimisha miaka 113 na kusema anaamini Mungu atamuweka aishi miaka mingi zaidi. 
“Najisikia furaha, kuwa na umri huu, najiona kijana, nafurahia mlo wangu wa viazi vilivyopondwa na nyama za porini, nalala muda wote ninapohitaji, na ninaamka mwenye nguvu, napenda kuishi miaka mingi zaidi ili niudhihirishie umma kuwa Mungu atabaki kuwa Mungu,” alisema Papa Sedela. 
Aliongeza kuwa kama Methuselah aliishi miaka 969, Mungu anaweza kumuacha aishi zaidi ya  miaka 113, na Nuhu aliishi miaka 950 ambayo alisema kwa Mungu sio mingi hivyo anaweza kumuacha naye akaishi hadi miaka 200.

No comments: