RASIMU YA KATIBA MPYA KUPIGIWA KURA SEPTEMBA 21

Wakati kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) likishinikiza Bunge Maalumu la Katiba lisitishwe haraka iwezekanavyo, Bunge hilo limejiandaa kuwasilisha Katiba inayopendekezwa Septemba 21.
Hatua hiyo ya Bunge Maalumu, inalenga kuwapa fursa wajumbe wa bunge hilo, kuipigia kura Katiba hiyo. 
Spika wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema hayo jana. Aliongeza kuwa hatua hiyo itadhihirisha kuwa kazi waliyopewa na taifa ya kuandika Katiba mpya, itakuwa imekamilika.
Hatua hiyo ya Bunge kufupisha ratiba zake, inatokana na uamuzi wa Serikali kuwa shughuli zote za bunge hilo, ziwe zimekoma ifikapo Oktoba 4 mwaka huu na sio Oktoba 31. 
Sitta abainisha kuwa majadiliano ndani ya Bunge hilo yatakamilika kesho kutwa Jumamosi na kuanzia Jumatatu ijayo kamati ya uandishi wa katiba, itaendelea na kazi yake ambayo wataifanya kwa wiki moja na baada ya  hapo watawasilisha rasimu  Septemba 21.
Ratiba inafafanua kuwa baada ya katiba inayopendekezwa kuwasilishwa, wabunge wataipitia kabla ya kuanza kupiga kura Septemba 26 mwaka huu.
 “Nafurahi kuwaambia kwamba jana katika kikao cha kamati ya uongozi, tumedhihirisha kwamba tunakwenda vizuri na kamati ya uandishi, ambayo imekuwa ikitazama mambo yanavyokwenda na mjadala ulivyoanza jana, tumejipanga kutupa rasimu ya mwisho tarehe 21 mwezi huu.
“Kwa hiyo ni dhahiri kabisa kwamba lengo tulilopewa na taifa la kutoa katiba inayopendekezwa tutalimudu ndani ya wakati huo,” alisema Sitta. 
Sitta alisema kwa sasa uongozi wa Bunge hilo, unaangalia utaratibu wa kupiga kura  kwa wale ambao wako nje ya Bunge kwa sababu mbalimbali ukiacha wale ambao walisusa hasa wale ambao wako hospitali, ambao kanuni zinawaongoza utakapofika wakati wa kupiga kura, waandaliwe utaratibu wa kufanya hivyo.
Alisema wanafanya hivyo, kwa sababu akidi inahusu wabunge wote, ambao waliteuliwa na  rais kuwa wajumbe wa Bunge hilo na wajumbe wengine ambao wameingia kwa nyadhifa zao.
Upigaji kura huo, pia utawahusisha wajumbe wa Bunge hilo ambao watakuwa safari nje ya nchi. Baadhi ya wajumbe wanaenda Hijja huko Mecca, Saudi Arabia.
Katika kuhakikisha kuwa wajumbe wengi wanachangia ndani ya muda ambao wamepewa, uongozi wa Bunge hilo ulitoa mwongozo wa namna ya kuchangia na Sitta aliwataka wajumbe kuhakikisha wanafuata muongozo huo ili kuokoa wakati.
“Jana kidogo tuliongelea lakini leo mtaona kuna muongozo tumeugawa, kila mmoja ahakikishe anao kwa sababu kiti kitaangalia tunakaa ndani ya muongozo huo, kwa leo nadhani na kesho kwa sababu  mjadala tuukamilishe kufikia siku ya Jumamosi hii inayokuja, kwa hiyo tutakuwa tunagawa miongozo hii kuwawezesha waheshimiwa wajumbe kujua tunalenga wapi,” alisema Sitta.
Mwongozo alioutoa jana ulihusu Sura ya 2,3,4,5  ambao uliandaliwa na sekretarieti. Alisema mwongozo huo ni  muhtsari wa maoni, ambayo yalitoka ndani ya kamati zote 12. Alisema kwa hali hiyo mwenendo huo, hautaruhusu kuibua upya mjadala uliokuwapo ndani ya kamati.
Sitta alifafanua kuwa kuna masuala mbalimbali ambayo rasimu ilisema na muhtasari kamati zilijielekeza na kufikia muafaka na sehemu hawakufikia muafaka. Aliwakumbusha wajumbe hao kuwa ni kazi yao sasa kuboresha yale yaliyopo  kwenye mwongozo huo.
Sitta alisema kuhusu mambo ya imani ya dini, kamati kadhaa zilisema ibara hiyo ibaki kama ilivyo kwenye rasimu ya katiba  na nyingine zikaongezea  kwamba uwepo utaratibu wa kutambua na kuruhusu sheria na vyombo vya dini, kutambuliwa kisheria.
“Sasa mjadala wa jana ulifikia mahali kwamba kidogo uharibu mambo kwa sababu tumerejea tena kuidai mahakama ya kadhi ndani ya katiba na wengine wanasema ndivyo ilivyo Uganda wakati sio kweli, Zanzibar sio kweli mahakama kama hiyo inatambuliwa ndani ya sheria, sio lazima ndani ya katiba.
 “Tunachotunga hapa ni kuandika katiba, sio sheria na kwa suala hili  hapa kwa Tanzania Bara Kamati ya Pamoja ambayo inasimamiwa na waziri mkuu imekuwa ikilishughulikia ili lifike mwisho wake, kwa hiyo kulirejea  tena na kusema kwamba ni jambo ambalo linazungumzwa ndani ya katiba sio sahihi,” alisema Sitta.
Kwa hali hiyo aliwaomba wajumbe, kuhakikisha kuwa hawarudii tena yale waliyoyajadili kwenye kamati. Alisema kama hoja ilishindikana na ikawekwa pembeni, kutokana na wajumbe kutofikia muafaka fulani; sio wakati wa kurejesha jambo hilo ndani ya Bunge, kwani kufanya hivyo ni kuanzisha upya mjadala  wakati kazi yao kwa sasa ni kuboresha kile ambacho kinaweza kuleta muafaka.
Kutokana na msimamo huo wa Sitta, baadhi ya wajumbe walimpinga na mjumbe wa kwanza kufanya hivyo, alikuwa ni Ezekiah Oluoch aliyetaka apewe mwongozo, kwa sababu kuna kifungu cha kanuni  kinachotoa fursa kwa mjumbe yeyote wakati wa mjadala, kuwasilisha marekebisho na maboresho au mabadiliko, ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo hayabadilishi msingi au maana.
“Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti tukiendelea tu na haya ambayo yamewekwa na kamati na tusiongezee vingine, tutakuwa na shida kwa sababu tayari ulishapokea malalamiko kwamba baadhi ya kamati hawakuweka hata vile  vifungu, ambavyo vilikuwa vimekubalika, kwa hiyo nilikuwa naomba nipate muongozo kwamba kwa nini hiyo haki mjumbe asiitumie iliyopo kwenye rasimu na badala yake tutumie muongozo tuliogaiwa  asubuhi ya leo?” alihoji Oluoch.
Akijibu hoja hiyo, Sitta alisema hilo ni jambo ambalo lipo wazi. Alionya kuwa taratibu wa kuleta mabadiliko ni kitu kimoja, ambacho kitafumbua mjadala upya.
Alisema mjadala huo ni kitu kingine na mambo yaliyokuwa ndani ya kamati ni kitu kingine. Alisema yeye anajielekeza kwenye hilo la pili kuanzisha mjadala,  ambao tayari kwenye kamati walishazungumza.
Mwenyekiti huyo alisema fursa za kuleta mabadiliko kwa maandishi, zinabaki palepale na hata hatua ya kusoma ile rasimu kamili kuanzia ibara ya kwanza hadi ya mwisho, ipo pale pale kwa mjumbe kuweza kupeleka pendekezo la mabadiliko ambalo linaweza kupigiwa  kura. 
“Kwa hiyo mimi sioni kama hayo mambo mawili yanapishana, hata kidogo, kuna kanuni za mjadala ambazo lazima tuzizingatie, hatuwezi kurudia kazi tulizofanya kwenye kamati kwa takribani wiki tatu tukairejesha kwenye mjadala, lakini kuleta mapendekezo ya mabadiliko inaruhusiwa,” alisema.
Waziri katika ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya alionya kuwa wajumbe walioko nje ya Bunge, ambao wanatarajia kuwa kuna katiba nyingine itaandikwa baada ya mwaka 2015, wamechelewa.
Alisema propaganda wanayoiendesha nje ya Bunge hilo  kuwa mchakato huo utaanza upya, hauna tija. Aliwahakikishia wananchi kuwa wajumbe wa bunge hilo, wamefanya kazi kwa weledi mkubwa na watawapatia wananchi katiba mpya.
Wakati huo huo,  viongozi wa Ukawa waliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam  jana na kuendelea kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete, atoe agizo mara moja la kusitishwa kwa vikao vinavyoendelea vya Bunge Maalum la Katiba.
Aidha umoja huo umependekeza katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, ifanyiwe marekebisho na kuwekwa kipengele kitakachotoa amri kwa utawala ujao, kuhakikisha unamalizia mchakato wa Katiba uliositishwa kwa kuendelea na hatua ya Bunge la Katiba.
Mwenyekiti Mwenza wa umoja huo, James Mbatia alisema katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni kati yao na Rais Kikwete, walikubaliana mchakato huo wa Katiba kwa sasa usitishwe.
“Tumeshakubaliana kimsingi kwamba mchakato huu wa Katiba hautaweza kufikia hatua ya mwisho kwa wakati huu ya uchaguzi, muda umekwenda sana na makubaliano hayo tumetiliana saini wote hadi wenzetu wa CCM, ila tunashangaa kwanini Bunge hilo hadi sasa linaendelea tena hadi Oktoba 4, haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma,” alisisitiza Mbatia.
Alisema katika makubaliano waliyoyafikia kwenye vikao hivyo, vilivyofanyika Agosti 31 na Septemba 8, mwaka huu, yalizingatia maoni ya wadau na kukubaliana kwa pamoja kuahirisha mchakato wa katiba ili kupisha maandalizi ya Bunge la kawaida.
“Hata hivyo, pamoja na makubaliano haya, sisi kama Ukawa msimamo wetu ni Bunge linaloendelea la Katiba lisitishwe ili tuanze kufanyia marekebisho Katiba ya sasa tuweze kufanya uchaguzi kwa maridhiano na amani,” alisema.
Alimpongeza Rais Kikwete kwa kuchukua uamuzi wa kukubali kukutana na umoja huo kwa mashauriano  hadi kufanikisha, hatua hiyo aliyoiita nzuri ya kuwezesha kupata muafaka wenye maslahi mapana kwa taifa, kuhusu suala la katiba na uchaguzi.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alimtaka Sitta kuacha kutumia vibaya fedha za umma na kusitisha mara moja Bunge hilo, vinginevyo kukitokea machafuko au vurugu zinazotokana na mchakato huo wa Katiba atalaumiwa yeye.
Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo kutoka CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema katika marekebisho ya 15 ya Katiba ya sasa, walichopendekeza ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, kuweka mgombea huru, Rais kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 50 na matokeo ya Urais kuhojiwa mahakamani.
Mwenyekiti wa Chadema na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, wakati akifungua uchaguzi wa Baraza la Vijana wa chama hicho Dar es Salaam jana, alisisitiza juu ya Bunge hilo kusitishwa mara moja kabla ya Oktoba 4, mwaka huu, vinginevyo wataingia barabarani.

No comments: