Ikiwa imebaki siku moja kufunguliwa kwa
pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014-15, mambo tayari yamenoga baada
ya kukamilika kwa safu ya waamuzi watakaochezesha mechi za ufunguzi wiki hii.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi
Tanzania, Silas Mwakibinga aliliambia gazeti hili jana, orodha ya waamuzi iko
tayari na kuwataka watakaochezesha katika michezo hiyo kutenda haki.
Katika mchezo wa Yanga dhidi ya Mtibwa
Sugar ya Mvomero, Morogoro, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri
itachezeshwa na mwamuzi Dominick Nyamisano kutoka Dodoma.
Wakati huo, mabingwa watetezi, Azam FC
itakuwa mwenyeji wa Polisi ya Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi,
Dar es Salaam katika mchezo utakaochezeshwa na mwamuzi Abdallah Kambuzi kutoka
Shinyanga.
Mwamuzi wa Dar es Salaam, Hashim Abdallah
atakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga kuziamua timu mbili ngeni
katika ligi msimu huu, wenyeji Stand United na Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Mgambo
JKT ya Tanga dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba utakaochezwa kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Kennedy Mapunda wa Dar es
Salaam.
Aidha, Ruvu Shooting ya Pwani itacheza na
Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi na kuchezeshwa na
mwamuzi David Paulo wa Mtwara.
Washindi wa tatu wa ligi hiyo msimu
uliopita, Mbeya City itawakaribisha JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya katika mchezo utakaochezeshwa na Mohamed Theophil wa Morogoro.
Baada ya michezo hiyo ya Jumamosi katika mchezo
wa Jumapili, Simba watakuwa ni wenyeji wa Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam, na mwamuzi Jacob Adongo wa Mara atachezesha.
Kwa mujibu wa Mwakibinga, waamuzi hao wa
kati ni miongoni mwa waamuzi wa kati 21 watakaochezesha ligi hiyo iliyopangwa
kufikia tamati Aprili 18, mwakani. Kutakuwa na waamuzi wasaidizi 46.
Mwakibinga alisema anategemea waamuzi hao
watachezesha mchezo huo kwa kufuata sheria 17 za soka bila kupendelea na kwa haki.
“Hiyo ndio orodha ya kwanza, kuna nyingine
itatoka kwani wapo wengi, na wasaidizi wao tayari, tuna imani watazingatia
maadili ya kazi yao,” alisema Mwakibinga.
No comments:
Post a Comment