WAUMINI WAMBURUZA KORTINI ASKOFU WAO


Askofu wa Kanisa  la EAGT Kanda ya Magharibi, Raphael  Machimu  amefikishwa mahakamani na waumini wa kanisa hilo. 
Uamuzi huo unatokana na kupinga kufukuzwa kwa Mchungaji wao  David Mabushi, wakisema hajafanya kosa lolote, zaidi ya uonevu, hivyo kusema hawakubaliani na jambo hilo. 
Waumini hao wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi mjini hapa, walisema wamemfikisha mahakamani askofu huyo kwa kuwa hakuna kipengele kilichoainishwa cha kumwondoa mchungaji bila kosa. 
“Tumeamua kumfikisha mahakamani Askofu Machimu kwa kumwandikia barua ya kumfukuza mchungaji wetu aondoke katika kanisa letu hivyo tumepinga na hatujafurahishwa na kitendo hicho ndio maana tukaenda ngazi ya mahakama ili ikaamue,”’alisema mmoja wa waumini hao. 
Aliongeza kuwa, kanisa hilo lilianzishwa mwaka 1992 likiwa chini ya mchungaji John Chambi ambaye aliondolewa na uongozi wa Jimbo la Shinyanga akiwepo Mchungaji Machimu ambaye wakati huo alikuwa Katibu wa jimbo hilo, lakini walikaa bila ya mchungaji hadi mwaka 1999 alipopatikana Mchungaji Moses Kuzenza ambaye kwa sasa ni marehemu. 
“Kwa kweli tumechoka kuondolewa ondolewa wachungaji mara kwa mara tumeamua sasa kwenda katika ngazi ya mahakama tuone kama mchungaji wetu Mabushi kama atakuwa na makosa ya kuondolewa katika kanisa la Majengo,” alisema mmoja wa waumini wa kanisa hilo. 
“Sisi ndiyo waumini wa hilo kanisa na ni waumini wa miaka mingi hakuna mali ya EAGT hata bati moja , mali iliyopo humo ni mali ya waumini, lakini kusema aondoke mchungaji aache mali ya EAGT kanisa hilo ni mali ya waumini,” aliongeza. 
Askofu Machimu hakupatikana kuzungumzia suala hilo. Hata hivyo, Kesi hiyo iliyoanza kutajwa Agosti 4 mwaka huu  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga na baadaye Agosti 14 mwaka huu, imeahirishwa hadi Agosti 25 mwaka huu kwa ombi la Wakili wa Mshitakiwa aliyeomba kupewa muda aweze kuelewa kiini cha kesi husika.

No comments: