Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amesema Katiba ya sasa
yenye miaka 50 imewezesha kutungwa kwa sheria
na kanuni zinazoleta maumivu kwa wananchi na kusema lengo la kutungwa
kwa Katiba mpya ni kuziba mianya hiyo.
Alipinga kauli za baadhi ya wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
na wananchi wengine wanaotaka bunge hilo livunjwe kwa maelezo ya kuokoa fedha,
akisema ni upuuzi kwani limeshafikia hatua ya mbali hivyo ni hasara kulivunja.
Sitta alibainisha hayo alipokutana na wakulima wa pamba kutoka mikoa 11
waliowasilisha kwake maoni ya wakulima wenzao wanayotaka yaongezwe kwenye
majadiliano ya rasimu ya katiba yanayoendelea mjini hapa.
“Katiba tunayotengeneza lazima izibe
mianya ya kuwaumiza wananchi na kuwadhibiti watendaji, mfano juzi Mwanza kuna
wakulima wamekaa hapo tangu mwaka 1970 sasa wameondolewa kwa kupigwa na kunyang’anywa nyavu zao. Lengo la
kutungwa katiba mpya ni iwe rafiki kwa wananchi wa kawaida,” alisema.
Sitta alipoulizwa kama ni sawa kisheria Ukawa kutoshiriki Bunge la maalumu
alijibu:
“Ukawa haijavunja sheria na si kosa kikanuni, siwezi kuwalaumu ila nyinyi
wananchi pimeni, wametumia njia hiyo kuonesha hisia zao, lakini inaleta
wasiwasi kuonesha sasa inakuwa tabia, kama unamuona mtu mpumbavu dawa si kususa
ila muelimishe.”
“Wao wanaona roho ya katiba ni serikali tatu nasi tunaona roho ya katiba ni
matakwa ya wananchi, sisi tuendelee kutunga katiba tuwaache wao wachache.
Mwenye kujibu hili ni wananchi wenyewe si hao wanaojiona wana akili sana,”
alisema.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Pamba (Tacoga), George
Mpandiyi aliyesoma maazimio ya wakulima
wa pamba, alisema wanataka vyama vya siasa vitambue wakulima wanataka Katiba
mpya haraka itatue matatizo yao hivyo wamemtaka mlezi wa chama chao, John Shibuda kuendelea kuhudhuria mjadala wa Bunge la Katiba.
Naye mwenyekiti wa chama hicho aliyeongoza msafara huo, Godfrey Mokiri
alitaja maoni yanayotaka yaingizwe kwenye rasimu ya katiba kuwa ni Haki ya
ardhi kwa wakulima na wafugaji ili kuzuia migogoro ya ardhi, haki za wakulima
kupata mikopo, ruzuku za pembejeo kwa wakulima na katiba izuie dhuluma
mbalimbali kwa wakulima na inapotokea walipwe fidia.
No comments:
Post a Comment