VIJANA WAJENGA MAJUMBA YA KISASA KUPITIA BODABODAJiulize unaweza kufanya nini na Sh 2,000 tu unayoikamata kwa siku? Kwa wengi, wanaweza kukiona kiasi hicho cha fedha kuwa ni kidogo mno, lakini si ukweli.
Na katika kuthibitisha hilo, kundi la vijana 100 waendesha bodaboda wamefanya mapinduzi makubwa ya kimaisha, baada ya kuamua kudunduliza kiasi hicho cha fedha kila siku, na sasa wakifikia hatua ya kumiliki majumba ya kisasa na hata vyombo vyao vya usafiri.
Kama ilivyo kwa vijana wengi waliovamia kazi hiyo wakitokea vijiweni walikosota sana kimaisha na hata kujikuta wakigeuka wakabaji, waokota chupa tupu za maji, wapiga debe, wazibua vyoo na kadhalika, hao nao walipitia maisha hayo.
Lakini baada ya kuchoshwa na uduni wa maisha, waliamua kutafuta njia halali ya kuajiriwa kama madereva wa bodaboda, lakini wakilenga kufika mbali zaidi.
Baada ya kuchoshwa na usumbufu wa askari wa vikosi wa usalama barabarani, vijana hao kutoka eneo la Kitengele, wilaya ya Kajiado inayopakana na Tanzania kwa upande wa mkoa wa Arusha, waliamua kuunda umoja wa kusaidiana.
“Ilikuwa mwaka 2009, tulichoshwa na kukamatwa na askari, kubambikiwa kesi na hata kunyang’anywa pikipiki. Tukaona tuanze kuchangishana fedha ili tuwe na akiba za kuweza kuwalipia faini wenzetu,” anaanza kusimulia Aloise Mwai,  Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Kitengela (KITEMOTO). 
Anasema haikuwa kazi rahisi kukusanya fedha kutoka kwa kila mmoja, lakini baada ya kuwaelimisha sana, wakati mwingine wakilazimishwa kutoa michango, walijikuta wakiingiza kiasi kikubwa cha fedha. 
“Kwa siku, kwa watu 100 tuliingiza Sh 200,000 hii ina maana kwamba kwa mwezi ni Sh milioni 6 na kwa mwaka Sh milioni 72. Haikuwa pesa ndogo na kufikia hatua hii, kila mmoja aliona kumbe inawezekana kwenda hatua kubwa zaidi kwa kusaidiana. 
“Tukaanza kukopeshana kununua pikipiki zetu. Hivi sasa kila mmoja anamiliki chombo chake cha usafiri, yaani pikipiki na wengine wamenunua hata magari. 
“Lengo hili lilipokamilika, tukaweka lengo la kupanda miti ili kupunguza vumbi katika mitaa ya Kitengela tunayofanyia kazi, mambo yakawa safi ingawa tunapambana na matatizo kadhaa, likiwemo la mbegu na umwagiliaji wa mara kwa mara. 
“Na lengo la tatu, lilikuwa kutafuta mashamba ili mwenye uwezo aweke hata kibanda chake, na hii ilitokana na sisi wenyewe, kutokana na kutoka katika historia isiyoridhisha kiuchumi. Wengi walikuwa wapigadebe, watu wasio na mbele wala nyuma kimaisha. Tulinuka shida tupu,” anasema kwa hisia kali kijana huyo aliyekuwa na dhamira ya kuwa rubani, lakini kutokana na kushindwa kufikia lengo, sababu kubwa ikiwa ni umasikini, aliishia kuwa mpigadebe na baadaye kondakta wa daladala. 
Anaongeza kuwa, baada ya wanachama kufikia mwafaka wa kutafuta shamba, walimvaa Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Isinya, Frank Maina aliyewashauri kuunda umoja (Kitengela Motorcycle Owners, yaani Kitemoto) uliokuwa na wanachama 200, ingawa wengine 100 waliachia ngazi. 
Na baada ya kila mwanachama kufikicha mchango wa Sh milioni 1.2, walinunua ekari 50 za ardhi katika eneo la Ngasemo, umbali wa kilomita 13 kutoka Kitengela katika barabara kuu ya Namanga-Kajiado, kwa kiasi cha Sh milioni 15 za Kenya, sawa na Sh milioni 270 za Tanzania. 
Kutoka kumiliki ardhi, walielekeza nguvu zao kwa Ushirika wa Ujenzi wa Nyumba Kenya (NACHU) uliowashauri jinsi ya kudunduliza na kuweza kujengewa nyumba za bei nafuu, lakini za kisasa kwa mkopo wa miaka saba. 
Kwa mujibu wa Katibu wa Kitemoto, Gathaga Maina, kwa makato ya miaka saba, kila mwanachama angekuwa na uhakika wa kumiliki nyumba ya karibu sh milioni 10 za Tanzania. Nyumba hizo ni za vyumba vitatu kimoja kikiwa na choo ndani, jiko, choo cha ndani kwa ajili ya wageni, choo cha nje na sehemu ya chakula.  
“Tuliona ni heri kuendelea kukamuana kiasi kile kile kila siku na hatimaye sasa kila mmoja wetu anafurahia kazi yake. Si ule utumwa na presha za kuhofia kama utatimiza hesabu za tajiri. Kila mmoja ana chombo chake, na kila mmoja ana uhakika wa nyumba na maisha kusonga mbele. Mungu atupe nini kama si mshikamano na busara tulizotumia? 
“Kwa sasa hakuna anayesikitika kwa kujibana na matumizi ya anasa kwa sababu tunachokifanya sasa ndio ukombozi wa maisha yetu. Naweza kusema tumefanikiwa, lakini bado mapambano dhidi ya maisha yanaendelea…,” anasema Maina. 
Mwanachama wa umoja huo, Peterson Mwangi aliyekuwa mchimba mashimo, anasema haikuwa kazi rahisi kujibana kifedha ili kuchangia katika umoja wao, lakini kwa sasa anamshukuru Mungu kwa miujiza aliyomtendea, akisema sasa ana unaheshimika na ana uhakika wa maisha. 
“Mwanzo nilikuwa mpigadebe kabla ya kujifunza kuendesha bodaboda nikiwa napeleka pesa kwa tajiri, lakini sasa daah…mimi ni tajiri na pia baba mwenye nyumba. Heshima imerudi sana na ninategemewa tofauti na siku za nyuma nilipogeuka mzigo na hata kuzua hofu kwa majirani wakiamini huenda pia ninajihusisha na udokozi,” anasema mwanachama mwingine, John Ndegwa. 
Baadhi ya nyumba zimekamilika. Wameshachimba visima vya maji na kuweka umemejua na matangi ya maji. Kwa ambao hawako tayari kuhamia, sasa wanaangalia uwezekano wa kukamilisha ujenzi ili wazipangishe kwa wanafunzi wa vyuo katika eneo hilo, Chuo Kikuu cha Theolojia cha KAG (Kenya Assemblies of God), Kampala International University (KIU) kampasi ya Kenya na chuo kipya kinachotarajiwa kujengwa wakati wowote kuanzia sasa. 
Aidha, wanachama hao wanaiomba serikali kuwaboreshea miundombinu ya eneo lao, ikiwa ni pamoja na kuwawekea barabara za lami. Pia wameomba kusaidiwa fedha kupitia mfuko wa barabara ili wamalize deni na kuanza hatua nyingine ya kuendeleza mradi wao. Kwa sasa umoja huo una wanachama 400. 
Kwa ujumla jamii ya Wakenya wamewamiminia sifa vijana hao kwa ubunifu wao. Na hakika, kilichofanywa na vijana hawa kinapaswa pia kuungwa mkono na vijana wengine, hasa wa Tanzania ambao hawaonekani kujitambua katika kazi yao hiyo, kwani hata umoja wanaouanzisha, unaonekana kubeba taswira za kisiasa zaidi kuliko kujikomboa kiuchumi.

No comments: