NGASSA KINARA WA MABAO LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Licha ya Yanga kutolewa mapema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mshambuliaji wake Mrisho Ngassa ndiye anayeongoza kwa upachikaji mabao mpaka sasa.
Michuano ya Ligi ya Mabingwa ipo hatua ya nusu fainali sasa ambapo  TP Mazembe ya Kongo (DRC)  itakutana na ES Setif ya Algeria na AS Vita ya Kongo pia  itakutana na CS Sfaxien ya Tunisia.
Yanga ilicheza raundi mbili za awali, dhidi ya Komorozine ya Comoro na dhidi ya Al- Ahly ya Misri.
Kwa mujibu wa taarifa ya tathmini iliyotolewa jana  kwenye mtandao wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Ngassa anaongoza kwa mabao sita.
Katika michuano hiyo, Ngassa alicheza mechi nne za raundi za awali ambapo katika mechi dhidi ya Komorozine alifunga mabao matatu katika kila mechi, nyumbani na ugenini na kufanya idadi ya mabao hayo sita.
Katika mechi ya nyumbani dhidi ya Al- Ahly, Yanga ilishinda bao 1-0 lakini ikatolewa kwa mikwaju ya penalti ugenini baada ya Ahly kupata bao moja na kufanya matokeo kuwa sare ya bao 1-1 na hivyo mechi kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Wanaomfuatia Ngassa kwa mabao ni Haithem Jouini (Esperance, Tunisia), Edward Takarinda Sadomba (Al Ahli Benghazi, Libya), Iajour Mouhssine (Raja Club Athletic, Morocco) na Knowledge Musona (Kaizer Chiefs, Afrika Kusini) wenye mabao matano kila mmoja ambao timu zao pia zimetolewa kwenye michuano hiyo.
Mubele Ndombe wa AS Vita ndiye pekee mwenye mabao matano na timu yake imekwenda nusu fainali.Wenye mabao manne ni Benyoussef Fakhreddine (Sfaxien, Tunisia), El Hedi Belameiri (E. S. Setif, Algeria,) na Abdelrahman Ramadan Fetori (Benghazi,) Abdoulaye Ssissoko (Stade Malien, Mali), Ahmed Akaichi (Esperance), Akram Djahnit (E. S. Setif), Cesair Gandze (AC Leopards, Kongo), Driss Mhirsi (Esperance), Etekiama Agiti Taddy (AS Vita) Kingston Nkhatha (Kaizer Chiefs,) na Lamine Diawara wa Stade Malien wana mabao matatu kila mmoja.

No comments: