Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limewakamata watu saba wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha mlemavu wa ngozi, Munghu Mugata (40) aliyeuawa kwa kukatwa mapanga nyumbani kwake usiku wa Mei 12 mwaka huu katika kijiji cha Gasuma, Kata Mwaubingi wilayani Bariadi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kudawa Yelema (52) ambaye ni mganga wa jadi, Sitta Maduhu (39), Jasamila Sungwa (42), Mpamba Saguda (18), Dede Madono (54), Majeshi Sunja (38), pamoja na Mabula Bindondo (52) wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Gasuma.
Akizungumza ofisini kwake jana, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapa, Paschal Mabiti (pichani), alisema kati ya watuhumiwa hao, mmoja ni mganga wa jadi.
Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na wasamaria wema, liliendesha msako mkubwa wa kuwasaka wahusika wa tukio hilo, ambapo lilifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa hao saba.
Alibainisha kuwa Madono, mmoja wa watuhumiwa hao, aliugua ugonjwa wa malaria wakati akiwa mahabusu na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi, ambapo alifariki dunia akiwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu.
Mabiti alieleza jeshi la polisi bado linaendelea kumsaka mdhamini wa mauaji hayo, pamoja na kutafuta sehemu viungo vya mlemavu huyo wapi vilipelekwa ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani na kujibu tuhuma zinazowakabili.
Aidha mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa marehemu Lughata alimwacha mtoto wake Tiri Kulwa (8) darasa la kwanza, ambaye alieleza kuwa kwa sasa mtoto huyo anahudumiwa na halmashauri ya Wilaya, ikiwemo kumsomesha. Hata hivyo, mkuu huyo alizitaka wilaya zote kuhakikisha wanakusanya takwimu sahihi za watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwa pamoja na kutambua mahali wanapoishi.
No comments:
Post a Comment