WACHINA WA 'SAMAKI WA MAGUFULI' WAACHIWA HURU


Baada ya kusota rumande kwa miaka mitano hatimaye raia wawili wa China waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kuvua samaki katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania bila kibali wameachiwa huru katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 
Aidha, mahakama imeamuru washitakiwa warudishiwe mali zao, ikiwemo meli iliyotumika kufanya uvuvi huo ikiwezekana na samaki walikutwa nao pamoja na hati zao za kusafiria. 
Kwa mara ya kwanza, walishitakiwa watu 35 kutoka mataifa tofauti ya Bara la Asia, kama vile China, Ufilipino, Vietnam na wawili raia wa Kenya, walikamatwa Machi 8, mwaka 2009 wakivua na walikutwa na tani 293 za samaki wakati huo, Dk John Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, hali iliyochangia samaki waliokamatwa kuitwa wa 'Magufuli’ hasa baada ya serikali kuamua kutaifisha meli na pia kugawa samaki kwa wananchi, vyuo na taasisi nyingine za umma. Kati ya washitakiwa hao, 35 waliachiwa huru na wawili kutiwa hatiani. 
Hakimu Mfawidhi Isaya Arufani aliwaachia huru washitakiwa hao jana baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo. 
Washitakiwa hao ni nahodha wa meli ya Tawaliq 1 iliyotumika kufanya uvuvi huo, Hsu Chin Tai na wakala wa meli hiyo, Zhao Hanquing. 
Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi Prosper Mwangamila akisaidiana na Wakili Tumaini Kweka, alidai kuwa, DPP amewasilisha hati ya kuwaondolea mashitaka washitakiwa hao kwa kuwa hana nia ya kuendelea kuwashitaki na kuomba ipokelewe mahakamani. 
Wakili wa Utetezi Kapteni Ibrahim Mapinduzi aliiomba mahakama washitakiwa warudishiwe mali zao vikiwemo vielelezo vinavyoshikiliwa Mahakama Kuu ambayo ni meli waliyokamatwa nayo. Wakili Mwangamila alidai washitakiwa watapewa mali zao isipokuwa meli mpaka watakapothibitisha ni wamiliki wa meli hiyo. 
Awali washitakiwa hao walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka 30 jela tangu Februari 23 mwaka 2012 baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwatia hatiani kwa kufanya uvuvi haramu. 
Machi 28 mwaka huu Mahakama ya Rufani iliwaachia huru baada ya kushinda rufaa yao ya kupinga adhabu ya kifungo hicho au kulipa faini ya Sh bilioni 20 iliyotolewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Hata hivyo washitakiwa walikamatwa tena na Machi 31 walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa upya mashitaka yao.

No comments: