Magwiji wa Real Madrid wamethibitisha
kuwa timu yao ndio miamba ya soka duniani, baada ya kuishinda timu ya Tanzania
XI kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbele ya Rais Jakaya Kikwete,
wachezaji hao wa zamani wa Real Madrid wakiongozwa na Luis Figo, walitandaza
soka ya kuvutia na kuwafurahisha maelfu ya mashabiki wa soka.
Real Madrid kwa sasa ndio miamba ya
soka Ulaya ikiwa imetwaa taji la 10 Mei mwaka huu, na miongoni mwa waliokuja,
wamechangia katika kupatikana kwa mataji hayo muhimu.
Mchezaji Ruben de la Red alikuwa mwiba
mkali kwa Tanzania XI ikiongozwa na wanasoka nyota wa zamani wa Tanzania, baada
ya kufunga mabao yote matatu likiwamo la penalti.
Bao pekee la Tanzania halikufungwa na
mchezaji wa nyota hao wa zamani wa Tanzania, bali alijifunga mchezaji wa Real
Madrid.
Bao la Tanzania XI lilipatikana katika
dakika ya 45, likifungwa na mchezaji wa Real, Roberto Rosas kutokana na kona
iliyochongwa na Mecky Maxime kutoka mashariki mwa uwanja.
Madrid walijipatia bao la kuongoza
katika dakika ya 15 likifungwa na Ruben de la Red kwa pasi ya nyota wa zamani
duniani, Figo.
Hadi mapumziko, Tanzania XI na Real
Madrid, zilikuwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili, Real Madrid
iliendeleza kutandaza soka ya kuvutia huku Figo akiwa mwiba mchungu kwa
Tanzania XI ambayo ilionekana kupwaya kipindi hicho.
Hali hiyo ilimpa mwanya De la Red
kufunga bao la pili kwa penalti baada ya Habib Kondo na Mtwa Kihwelo, kumchezea
dhambi mmoja wa wachezaji wa Real, mfungaji kupiga penalti nzuri iliyompita
kipa Peter Manyika.
Kama hiyo haitoshi, mchezaji huyo
alifunga bao la tatu baada ya kuwapiga chenga walinzi wa Tanzania XI na kipa
wao Manyika, na kukwamisha mpira wavuni.
Bao hilo lilimfurahisha Rais Kikwete
na viongozi wengine wa jukwaa kuu ambao walicheka sana kutokana na jinsi
lilivyofungwa, huku wachezaji wa Tanzania wakiwa wameanguka chali.
Kipindi cha kwanza, Dua Said
aliifungia Tanzania XI, lakini bao hilo lilikataliwa.
Mbali ya Figo aliyekuwa Mwanasoka Bora
wa Ulaya mwaka 2000 na Mwanasoka Bora Duniani mwaka 2001, pia alikuwapo nyota
Christian Karembeu katika kikosi cha Madrid.
Awali, Tanzania XI ilianza na kipa
Mohammed Mwameja na miongoni mwa wachezaji waliocheza jana kwa upande huo, ni
manahodha wa zamani wa Stars, Shadrack Nsajigwa, Mecky Maxime na Salum Sued
‘Kussi.’
Wengine waliocheza ni Yusuf Macho,
Habib Kondo, Dua Said, Abubakari Kombo, Athumani China, Mtwa, Shaaban
Ramadhani, Sabri Ramadhani, Kally Ongala, Madaraka Selemani, Stephen Nyenge,
Mao Mkami, Emmanuel Gabriel, Nassoro Bwanga, Abdul Maneno.
Katika mechi hiyo, timu zilikaguliwa
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara, wakati
Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi uwanjani hapo.
Mwishoni mwa pambano, alikabidhi kombe
kwa De la Red na kisha akamkabidhi mpira kwa kufunga mabao matatu, huku akiweka
saini yake.
Magwiji hao wa Real Madrid ambao wako
nchini kwa mwaliko wa Kampuni ya TSN inayomilikiwa na Farough Baghozah, leo itakwenda
mkoani Kilimanjaro kutembelea Mlima Kilimanjaro.
Kesho itakuwa mkoani
Arusha katika mbuga ya Ngorongoro, na itarejea Dar es Salaam na kuondoka
Jumanne ijayo kurejea makwao.
No comments:
Post a Comment