Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na
wamiliki wa daladala mkoa wa Dar es Salaam wameunganisha nguvu zao kwa
pamoja kwa lengo la kuendesha mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART).
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika mkutano wa wamiliki wa daladala Mkoa wa
Dar es Salaam uliofanyika Ukumbi wa Karimjee, ukiwa umeandaliwa na kamati teule
ya wamiliki wa daladala jijini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa vyama vya wamiliki wa daladala
vya DARCOBOA na UWADAR, Sabri Mabruki na William Masanja, walisema kuwa
wameamua kuunganisha nguvu na UDA ili kuweza kumudu ushindani na makampuni
makubwa yatakayokuja kutoka nchi zilizoendelea hususan Ulaya na Marekani katika
mradi wa DART.
“Waswahili wanao msemo kwamba Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,
hatuwezi kushinda zabuni ya kuendesha DART kama tutakwenda tukiwa tumegawanyika
kama tulivyo sasa, yaani UDA kivyao na sisi DARCOBOA na UWADAR kivyetu hatufiki
popote, DART itachukuliwa na wazungu,” walisema.
Wakitoa maoni yao kuhusu uamuzi huo baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam
wamewapongeza wamiliki wa daladala pamoja na UDA kwa kuunganisha nguvu zao kwa
lengo la kumiliki uchumi wa nchi yao kama wazawa wa nchi hii.
“Hii ni nzuri kwani tunakaribisha
maendeleo kwa pamoja, suala la ubinafsi siku zote ndilo linalokwamisha ukuaji
wa uchumi, hivyo basi ni wazi kuwa uamuzi huo licha ya kuwafaidisha wamiliki
pia utawanufaisha na Watanzania wengine kwa kupata ajira na wakazi wa Dar es
Salaam kuwa na usafiri bora,” alisema Rayness Tegemeo.
No comments:
Post a Comment