MKAZI WA MAKONGO JUU ATUHUMIWA KULAWITI


Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Msose Michael (35) mkazi wa Makongo Juu Jijini Dar e Salaam kwa tuhuma za kuwalawiti mabinti wawili ambao aliwachukua kwa wazazi wao kwa ajili ya kazi za ndani. 
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kuwekewa mtego kutokana na vitendo vyake hivyo. 
Kamanda Mwambalaswa alisema tukio hilo lilitokea Agosti 21 mwaka huu majira ya saa 12 jioni huko mtaa wa Zogowale wilaya ya Kibaha. 
“Mtuhumiwa huyo aliwachukua mabinti hao ambao majina yao yamehifadhiwa wenye umri kati ya miaka (16) na (12) ambao aliwachukua huko Nachingwea mkoani Lindi kwa nyakati tofauti na kukaa nao nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam kisha kuwapeleka shambani kwake Zogowale,” alisema Kamanda Mwambalaswa. 
Alisema kuwa mabinti hao wakiwa shambani kwake walikuwa wakiangalia bata, kuku, kanga na mbuzi. 
“Mtuhumiwa alikuwa akilala nao chumba kimoja kila alipokuwa akifika kwenye shamba lake na kuwafanyia mchezo huo, hali ambayo iliwaharibu sana mabinti hao ambapo polisi waliweka mtego baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema,” alisema Kamanda Mwambalaswa. 
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa wakati akitoka kumpeleka mmoja wa mabinti hao hospitali kufuatia kulalamika kuwa anaumwa tumbo. 
“Baada ya kukamatwa mtuhumiwa, mabinti hao walipelekwa kituo cha Afya cha Mlandizi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na kugundulika kuwa walifanyiwa vitendo hivyo vya kulawitiwa,” alisema Kamanda Mwambalaswa. 
Aidha aliwataka watu kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo kama hivyo vya ukatili kwa watoto ili wachukuliwe hatua kali za kisheria, kwani ni kuvunja haki za binadamu na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi wa tukio hilo kukamilika.

No comments: