MASUALA YA KADHI, URAIA PACHA YAPATIWA UFUMBUZI


Kamati ndogo ya Uongozi ya Bunge Maalumu la Katiba iliyoundwa na Mwenyekiti Samuel Sitta, kupatia ufumbuzi masuala manne ambayo kamati nyingi zimeshindwa kufikia muafaka, imeyapatia ufumbuzi mambo mawili. 
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndogo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu Hassan alisema mambo hayo ni Mahakama ya Kadhi na uraia pacha. Hata hivyo, hakuwa tayari kuingia kwa undani juu ya ufumbuzi uliopatikana. 
Kwa mujibu wa Samia, mambo ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na kamati yake inayoundwa na watu 10, watano kutoka Zanzibar na watano kutoka Tanzania bara, ni Muundo wa Bunge ikiwemo kuangalia mambo ya muungano na kamati ya pamoja ya fedha ya muungano. 
Katika kuyapatia ufumbuzi masuala hayo, Sitta amewaalika Mhadhiri maarufu wa masuala ya Katiba, Profesa Issa Shivji kuzungumzia muundo wa muungano, wataalamu kutoka Uhamiaji na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa ajili ya masuala ya uraia pacha na makatibu wakuu wa wizara ya fedha na magavana wa Benki Kuu kuzungumzia masuala ya kamati ya pamoja ya fedha ya muungano. 
Samia alisema, “baada ya kumaliza kazi hiyo ya kutafuta ufumbuzi kwa mambo hayo manne tutawasillisha mapendekezo yetu kwenye kamati ya Uandishi kwa ajili ya kuyazingatia kwenye rasimu ya katiba”. 
Samia alitoa maelezo hayo baada ya kupokea maoni ya Chama cha Wavuvi nchini(TAFU) kutoka kwa wanachama wake waliowasilisha ofisini kwake jana na kusema bado kuna muda kwa makundi mbalimbali kuwasilisha maoni yao kuboresha rasimu ya katiba. 
“Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ipo kimya kwenye masuala hayo, hivyo hatuna kikwazo kupokea maoni na tumekubaliwa kupokea maoni mapya,” alisema. 
Tafu imewasilisha mambo 17 wanayotaka yaingizwe kwenye rasimu ya katiba kwa ajili ya maslahi ya wavuvi nchini na miongoni mwao kwa mujibu wa msemaji wao na Mratibu, Sijaona James, wavuvi wanataka kumiliki ardhi katika maeneo ya uvuvi na kuwa na uwakilishi kwenye bunge na baraza la uwakilishi. 
Sijaona alisema uvuvi unategemewa na watu milioni 10 nchini na Samia mbali na kuwashukuru wanachama hao kwa kuwasilisha maoni yao, lakini akawaeleza kuwa sio kila kitu walichowasilisha kitaingizwa kwenye rasimu hiyo.

No comments: