WATENDAJI WAWILI WILAYA YA BAHI MATATANI

Maofisa watendaji wa vijiji viwili katika Wilaya ya Bahi, wameingia matatani baada ya kutafuna fedha za michango ya wananchi zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa maabara za shule za sekondari.
Watendaji hao ni Killian Makota wa Kijiji Nhinyila Kata ya Mwitikila na  Issa Rashid wa  Kijiji cha Msisi Kata ya Msisi.
Hali hiyo ilitokana na madiwani wa Kata hizo, kutoa malalamiko juu ya watendaji hao katika kikao cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika wilayani humo jana.
Akitoa malalamiko hayo, Diwani wa Kata ya Mwitikila, Jamal Shabiby alidai kutokana na Makota kula fedha za michango ya wananchi, wananchi wamegoma kuchangia tena kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa maabara.
“Mimi ninaomba kabla ya kuendelea kuwahimiza wananchi kuendelea kuchangia ujenzi wa maabara, kwanza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mtendaji wa Kijiji cha Nhinyila kutokana na kula fedha za michango ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Msisi, Chuga Mgaliwa alidai mtendaji wake ametafuna zaidi ya Sh. milioni moja, ambazo ni michango ya wananchi.
Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa alisema Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Msisi, tayari ameshachukuliwa hatua, ikiwemo kuwekwa mahabusu.
Alisema baada ya Mtendaji huyo, kuwekwa mahabusu  aliamriwa kulipa fedha zote anazodaiwa Sh 800,000 ndipo atolewe. Hata hivyo, alilipa Sh 600,000 na akaomba aachiwe ili fedha nyingine akakope benki.
Mkwasa alisema mtendaji huyo, tayari ameanza utaratibu wa kukopa fedha benki ili amalizie Sh 200,000 zilizobaki.
Kuhusu Ofisa Mtendaji wa Nhinyila, Ofisa Utumishi wa Wilaya  ya Bahi, Fredrick Kayombo alisema wameshaanza kushughulikia tuhuma hizo, ikiwemo kumchukulia hatua za kisheria. Alisema katika mahojiano ya awali, mtendaji huyo alidai alivamiwa na kuibiwa fedha hizo.

No comments: