Rais Jakaya
Kikwete, ameagiza mamlaka zote za uhakiki wa mipaka na uwekaji mawe katika
Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Burundi na mipaka na nchi nyingine,
kukamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo.
Aidha,
amesema kuwa Tanzania inapima mpaka wake na Burundi na mipaka yake na nchi
nyingine jirani, si kwa sababu ya kuwepo kwa migogoro na nchi jirani, bali kwa
sababu ya kuwahakikishia wananchi wa nchi zote kufahamu ni sehemu gani na
mazingira yapi wanafanyia shughuli zao za maendeleo.
Rais
Kikwete ameungana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza juzi kuzindua kazi ya
upimaji na uwekaji mawe ya mpaka kati ya Tanzania na Burundi, katika sherehe kubwa
na ya kusisimua iliyofanyika upande wa Tanzania wa kijiji cha mpakani cha
Mugikomero.
Aliwasili
Mugikomero saa 8:15 mchana, akitokea Uwanja wa Ndege wa Mchauru, mjini Geita,
ambako ndege yake ilitua saa nne kamili asubuhi, ikitokea mjini Dodoma na kujiunga
na Rais Nkurunzinza ambaye alitangulia kuwasili kwenye kijiji hicho.
Rais
Kikwete ameelezea uzinduzi huo kuwa kielelezo tosha cha uhusiano mwema, udugu
na urafiki uliopo kati ya Tanzania na Burundi; nchi mbili ambazo pamoja na
Rwanda zilikuwa nchi moja chini ya utawala wa Wajerumani ulioitwa German East
Africa.
Nchi
hizo zilitengana baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia,
ambapo Tanganyika iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza wakati Burundi na
Rwanda ziliwekwa chini ya himaya ya Ubelgiji.
Akizungumzia
umuhimu wa kuhakiki mpaka, Rais Kikwete alisema mara ya mwisho kwa mpaka wa
Kimataifa wa Tanzania na Burundi kuhakikiwa na mkataba kusainiwa kati ya nchi
hizo, ilikuwa Agosti 5, 1924; miaka 90
iliyopita.
“Kama
zilivyo nchi nyingine za Afrika, Tanzania na Burundi zilirithi mpaka uliopo
kutoka kwa waliokuwa watawala wetu enzi za ukoloni. Mpaka huu haujafanyiwa
marekebisho wala kuimarishwa tangu nchi zetu zipate uhuru zaidi ya miaka 50
iliyopita.
“Katika
kipindi hicho, yamekuwepo mabadiliko mengi ikiwemo ongezeko la watu, shughuli
za maendeleo katika maeneo ya mpakani na hata alama za mipaka zimekuwa vigumu
kutambulika, ama kwa sababu ya kuchakaa au mawe yameng’olewa,” amesema Rais
Kikwete.
Aliongeza
pia kuwa baada ya kutambua vyanzo vya migogoro na utata miongoni mwa baadhi ya
nchi za Afrika, Umoja wa Afrika (AU) katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za Serikali
kilichofanyika Accra, Ghana Juni 2007, iliamuliwa kuwa nchi zote zishirikiane
kuimarisha mipaka yao ifikapo 2012. Muda huo uliongezwa hadi 2017.
Rais
Kikwete alisema kuwa zoezi hilo ambako katika awamu ya kwanza kilometa 120 za
mpaka zimepimwa na kuwekewa mawe ya utambuzi wa mpaka, halikuwa rahisi kwa
sababu mpaka wa Tanzania na Burundi ni mrefu, kiasi cha kilometa 450, sawa na
urefu kati ya Dar es Salaam na Lindi.
“Isitoshe
mpaka hauko mijini, maeneo mengi yako misituni kwenye mabonde na milima. Ni
vigumu kuyafikia. Kwa upande wetu, mpaka uko katika mikoa miwili ya Kagera na
Kigoma na katika wilaya tano, nne zikiwa katika Mkoa wa Kigoma na moja ikiwa
Ngara, Mkoa wa Kagera. Isitoshe, hatuna mfadhili na zoezi hili tumeligharimia
sisi wenyewe,” alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete alisema kuwa mbali na Burundi, Tanzania inaendelea na upimaji kwa nchi
nyingine jirani na kuongeza kuwa mpaka wa Tanzania na Kenya, Msumbiji na Comoro na Shelisheli
katika Bahari ya Hindi imekamilika na mikataba imesainiwa.
No comments:
Post a Comment