HALMASHAURI ZAAGIZWA KUNUNUA NYUMBA ZA BEI NAFUU NHCHalmashauri nchini zimetakiwa kununua nyumba za bei nafuu zinazojengwa na Shirika la Nyumba (NHC) ili kuwapangisha watumishi wake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizindua mradi wa nyumba nafuu katika eneo la Nyakongo wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya maeneo watumishi wa halmashauri kukaa mbali na sehemu zao za kazi kwa visingizio vya kukosa makazi.
Alisema sababu hiyo sasa haina msingi katika maeneo ambayo NHC imejenga nyumba zao kwani halmashauri inaweza kununua nyumba hizo na kuwapangisha watumishi wake.
Hawa NHC wana utaratibu kwa kupitia mabenki wanayoshirikana nayo hivyo kwa kutumia utaratibu huo halmashuri mnaweza kwenda katika hizo benki na kuingia mkataba na kukopa nyumba hizo na kisa kuwapangishawatumishi…’’ alisema.
Aidha Rais Kikwete alisema shirika hilo linafanya kazi nzuri katika ujenzi wa nyumba hizo za bei nafuu huku akilitaka kuongeza zaidi idadi ya nyumba.
Alisema ni vyema sasa halmashuri zikaongeza maeneo ya kujenga nyumba hizo ili wananchi wengi zaidi waweze kuishi katika nyumba bora.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa NHC Nehemia Mchechu alisema mradi huo ni utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Alisema mradi huo wenye nyumba 44 hadi kukamilika utakuwa umegharimu Shilingi bilioni 1.2.
Alisema nyumba hizo zinauzwa kwa gharama kati ya Sh milioni 35 hadi 40 kulingana na ukubwa wa nyumba husika.
Hata hivyo alisema bado kuna tatizo la kodi katika uuzaji wa nyumba hizo na ndio kinachofanya kuuzwa kwa bei kubwa.
Alimuomba Rais kusaidia katika kusukuma nia ya kushusha kodi ili nyumba hizo ziuzwe kwa bei nafuu na kila mwananchi aweze kununua.

No comments: