WATAALAMU WAELEZEA UDHAIFU WA RASIMU YA KATIBA



Wataalamu wa fedha kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wamebainisha hatari ya kufuata Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa upande wa masuala ya fedha.
Wakitoa elimu kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba jana mjini hapa, wataalamu hao wa fedha  ambao ni Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha wa pande zote, Magavana wa Benki Kuu (BoT) na Wahasibu Wakuu wameonesha upungufu kwenye Rasimu hiyo kwenye upande wa madaraka ya Benki Kuu.
Mjumbe wa Bunge hilo kutoka Kamati namba Moja, Evod Mmanda aliyehudhuria semina hiyo ya kupewa elimu juu ya masuala ya fedha pamoja na Mfuko wa pamoja wa fedha aliliambia gazeti hili kuwa “Wataalamu wametuambia huwezi kuigawanya Benki Kuu na duniani kote kwenye Muungano hakuna sehemu ya kuigawa benki hiyo.
 “Sasa Rasimu ya Katiba inaeleza nchi washirika zitakuwa na benki zake zenye kufanana na Benki Kuu wakati kitaalamu Benki Kuu inakuwa moja na yenyewe ndiyo inayoratibu mikopo, inasimamia taasisi za fedha, inayopanga riba na inayosimamia uchumi.”
Kasoro nyingine iliyobainishwa na wataalamu hao wa fedha ni kwamba Rasimu imeweka rasilimali nyingi kwenye nchi washirika na kuifanya Serikali ya Muungano kuwa dhaifu hivyo haitakuwa na fedha na itashindwa kusimamia uchumi jambo ambalo wamesema ni hatari kwa nchi.
Kuhusu deni la Taifa alisema hali ya Tanzania ni nzuri kwani kwa sasa limefikia asilimia 40 ya pato la Taifa wakati Japan ni asilimia 250 na Marekani asilimia 100 ya pato la taifa na kufafanua “Deni letu kwa sasa ni asilimia 19 hadi 20 lakini imefikia asilimia 40 kutokana na madeni ya nyuma na kwa sasa mengi tunayolipa ni ya miaka 1965 hadi 1970, wananchi wanapotoshwa kabisa hali si mbaya.”
Alisema wataalamu hao wameonesha kwamba katika Muungano wa sasa hakuna upande unaonyonya mwenzake tofauti na watu wanavyodhani kuwa Zanzibar inanyonywa kwenye Muungano.
Kwa upande wa Mjumbe Hamisi Dambaya kutoka Kamati Namba Tano, alisema wataalamu hao wamewaeleza wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba waliohudhuria semina hiyo kuwa pande za Bara na Zanzibar zipo kwenye mazungumzo ya hatua ya juu kuhusu kuanza kwa Mfuko wa Pamoja wa Fedha na siku si nyingi inaweza kuanza kazi.
Kuanza kwa Mfuko huo kutaondoa malalamiko ya sasa kuwa upande wa Zanzibar haupati mapato yanayostahili kwani kuna mfuko mmoja wa fedha na Zanzibar inapewa asilimia 4.5 ya mgawo wa fedha hizo.
Chini ya Mfuko huo kila upande utaonesha kiwango cha mapato inayokusanya na jinsi itakavyochangia kwenye Muungano.
 “Hata huo mgawanyo wa asilimia 4.5 inayopewa Zanzibar imeonekana ni kubwa kutokana na idadi ya watu wake kidogo…,”alisema mjumbe huyo.

No comments: