WATAKA BUNGE MOJA LENYE CHEMBA ZA BARA, ZANZIBAR NA MUUNGANO


Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba wametaka kuwepo Bunge moja lenye sehemu tatu kwa kutenganisha majadiliano ya mambo ya Zanzibar, Tanzania Bara na Masuala ya Muungano huku wakiona hakuna haja ya Bunge kuthibitisha viongozi wote wa serikali.\
Sambamba na hilo, wabunge hao wamepokea maoni kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inayotaka kwenye katiba waruhusiwe kuwashughulikia wahujumu uchumi badala ya sasa ya kukamata watoaji na wapokeaji rushwa pekee. 
Kamati namba tatu inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Michael Francis imetaka muundo wa Bunge uwe wa Bunge moja na kuwe na sehemu tatu kwa wabunge kutoka Zanzibar wajadili masuala yao, Tanzania bara nao wajadili yao na wakutane kwa pamoja kujadili masuala la Muungano tofauti na ilivyo sasa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanajadili masuala ya Zanzibar na wanakutana na wabunge wa Tanzania bara kujadili masuala ya bara na muungano kwa pamoja. 
Dk Francis alisema wabunge hao watapatikana wawili kwa kila jimbo kwa kuzingatia jinsi yaani atasimama mwanamke na mwanaume.
“Pia tumepokea maoni kutoka wananchi na taasisi na kuziongezea sura zake na miongoni mwao ni Takukuru waliotaka sasa wawekwe kwenye katiba kuweza kushughulikia uhujumu uchumi na si kuachiwa kukamata watoa na wapokea rushwa pekee”, alisema Dk Francis.
Kwa upande wa Kamati namba 10, Mwenyekiti wake Anna Abdallah alisema wamekubaliana serikali mbili kama ilivyo sasa, lakini nafasi ya viti maalumu ifutwe na kila jimbo kuwe na wagombea wawili, mwanamke na mwanaume ili kufikia uwiano wa asilimia 50 kwa wanawake na wanaume. 
Hata hivyo, maamuzi yote wamekubaliana kwa wingi wa kura bila kuangalia theluthi mbili ya kura kwa bara na Zanzibar kwa sababu akidi haikuweza kutimia kwa wajumbe kutoka Zanzibar. 
Kuhusu viongozi kuthibitishwa na bunge, alisema kamati yake imeipinga rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba kwani imetaja watu wengi wathibitishwe na bunge na wao kuwapunguza na kubakiza Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwani hao utendaji wao unaingiliana na bunge. 
“Bunge si mwarobaini wa mambo yote hata kila mtu athibitishwe, taasisi zithibitishe watu wao, haiwezekani Jaji Mkuu athibitishwe na bunge, sisi tunaona ni kuingiliana kwa mihimili wakati kazi yake hatuna mamlaka nayo. Unakuta rasimu inasema Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi athibitishwe na bunge wakati kazi yake ni kusimamia bunge sasa huyo si atajipendekeza kwa wabunge…tunataka mgawanyo wa kazi za mihimili,” alifafanua Anna.
Aliongeza kuwa, mawaziri waendelee kuwa wabunge ili waweze kubanwa wanapokosea na kusisitiza: “tunataka kuwatoa jasho na kuwabana kwenye mambo kadhaa lakini wasipokuwa wabunge watakuwa mbali tutashindwa kuwapata”.
Kamati hiyo Namba 10 ilitaka Rais wa Zanzibar awe makamu wa rais na kuundwe tume kisheria ya kushughulikia kero za muungano ambapo mwenyekiti wake awe makamu huyo wa rais. 
Kuhusu mgombea urais, Anna na Dk Francis walisema kamati zao zimekubaliana awe yeyote mwenye kuanzia miaka 40 na mwenye uwezo wa kiakili bila kuwa na ukomo wa umri.

No comments: