Serikali
imeanza kuingiza nchini vifaa vya kuwabaini watu wanaohisiwa kuwa na dalili za
ugonjwa wa homa kali ya ebola ambavyo vitawekwa kwenye viwanja vya ndege pamoja
na baadhi ya maeneo ya mipakani.
Jana Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe alikabidhi mashine nne za
kuwapima abiria wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege bila kuwagusa.
Vifaa hivyo vinabaini mtu kuwa na dalili za ebola kutokana na joto lake na
abiria wanapimwa kwa kumulikwa machoni na kwenye masikio.
Kwa kuanzia
mashine hizo ambazo ni mfano wa kamera
zitapelekwa kwenye viwanja vya ndege vya Mwanza, Kilimanjaro, Zanzibar
na Dar es Salaam. Maeneo hayo kwa mujibu wa naibu waziri huyo ndiyo yanapokea
wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi.
Dk Kebwe pia
aliagiza shehena ya mashine zingine zitakazoingizwa nchini kuanzia leo
zipelekwe kwenye viwanja vingine vya Mtwara, Kigoma na maeneo ya mipakani
kuhakikisha kuwa kila abiria anayetoka nje ya nchi anapimwa dalili za ugonjwa
huo hatari.
Pia aliagiza
wanadiplomasia na viongozi wa kitaifa wanaotoka nje ya nchi ambako wanakwenda
kuhudhuria mikutano mbalimbali pia wapimwe kwani ugonjwa hauchagui cheo wala
fedha na hadhi aliyo nayo mtu.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani alisema jana kuwa
wamenunua mashine hizo nne kutoka Afrika Kusini, lakini zimetengenezwa nchini Marekani kwa kiasi cha
Sh milioni 16.
Alisema
katika kipindi hiki ambacho kuna mlipuko wa ugonjwa wa ebola huko Afrika
Magharibi, upatikanaji wa vifaa hivyo ni adimu na haiwezekani kupata mashine
zote kwa msambazaji mmoja, hivyo akasema leo ziwawasili mashine nyingine mbili
kutoka Ubelgiji.
Mkurugenzi
wa Manunuzi wa MSD, Heri Mchunga alisema mashine hizo kitaalamu zinajulikana
kama thermo scanners ni mashine za mkononi na kila abiria atakayeshuka uwanja
wa ndege atapimwa kwenye macho au masikio bila kugusana.
No comments:
Post a Comment