Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake
italipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo sugu la ugomvi kati ya wakulima na
wafugaji katika Mkoa wa Morogoro ambalo kimsingi linasababishwa na wachungaji
kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Aidha, amewataka wachungaji kuacha mara moja tabia yao ya
kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima akisisitiza kuwa
hicho ndicho chanzo cha ugomvi kati ya makundi hayo mawili.
Rais Kikwete ambaye anafanya ziara ya siku saba katika
Mkoa wa Morogoro ametoa ahadi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa ugomvi kati ya
makundi hayo baada ya kulalamikiwa kila aliposimama na wananchi kuhusu tabia ya
wafugaji kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima.
Akiwa njiani kutoka Ifakara, Wilaya ya Kilombero kwenda
Wilaya ya Morogoro, Rais Kikwete ameshuhudia mwenyewe malalamiko hayo ya
wananchi dhidi ya tabia hiyo ya wafugaji ambao wengi wao sio wakazi ama wenyeji
wa Mkoa wa Morogoro.
Baada ya kujaribu kuwaeleza wananchi katika maeneo mbali
mbali kuhusu chanzo cha ugomvi huo na nini hasa ufumbuzi wa suala hilo, Rais
Kikwete amewaambia wananchi katika Kijiji cha Mgalegole-Mngazi, eneo la
Duthumu, Tarafa ya Bwakila: “Nakwenda sasa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa
tatizo hili. Ni lazima tukomeshe tatizo hili.”
Alisisitiza: “Kimsingi, huu ni ugomvi usiostahili kwa
sababu kila mmoja kati ya makundi haya anamhitaji mwenzake. Wafugaji wanahitaji
chakula…ugali na mchele...kutoka kwa wakulima. Nao wakulima wanahitaji
kitoweo…nyama kutoka kwa wafugaji. Kubwa hapa ni wafugaji kuacha kulisha
ng’ombe kwenye mashamba ya watu wengine.”
“Mnawaachia watoto kuchunga ng’ombe. Wanaingiza mifugo
katika mashamba ya watu. Wakiwauliza mnawapiga, mnawajeruhi. Acheni mambo
haya.”
Rais Kikwete alianzia ziara yake juzi kwa kuweka jiwe la
msingi katika upanuzi wa Kituo cha Afya Kibaoni, mjini Ifakara, ambacho
kinapanuliwa kuwa Hospitali ya Wilaya na baadaye akakabidhi madawati 278 kwa
shule 17 za msingi za Tarafa za Mang’ula na Kidatu katika Wilaya ya Kilombero.
Madawati hayo yametolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi (TANAPA).
Baadaye, Rais Kikwete anayefuatana na mkewe, Mama Salma
Kikwete katika ziara hiyo alipanda treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na
Zambia (TAZARA) kwenda Kisaki, Wilaya ya Morogoro, ambako amelakiwa na mamia
kwa mamia ya wananchi.
Rais Kikwete pia alizindua Mradi wa Maji wa Duthumu
uliofadhiliwa na wanachama wa Lions Clubs za Sweden na pia kuzindua vifaa na
huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya katika eneo hilo.
Katika mji mdogo wa Mtamba, Rais Kikwete alizindua soko
jipya la kisasa na kuzungumza na wananchi ambako aliahidi kuwa Serikali imeanza
kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Bingwa-Mvua kwa kiwango cha
lami.
No comments:
Post a Comment