Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa onyo
pamoja na kutoza faini ya takribani Sh
milioni 5 kwa kituo cha redio na televisheni cha Clouds, kwa kukiuka kanuni za
utangazaji za mwaka 2005.
Wakielezea uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, Kamati
ya Maudhui ya mamlaka hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Margaret Munyagi ilisema
kuwa ukiukwaji wa kanuni hizo ulifanywa kwa nyakati tofauti na vituo hivyo.
Alisema kwa upande wa kituo cha redio cha Clouds, kupitia
kipindi chake cha ‘Njia Panda’ kilichorushwa hewani Juni 15 mwaka huu kati ya
saa 8.00 mchana na saa 10.00 jioni kilikuwa na mada iliyohusu safari ya kuzimu
ambapo maudhui yake yalijaa simulizi za kufikirika, za kishirikina na kichawi.
Aidha alisema kosa lingine kituo hicho hakikufuata kanuni
za Utangazaji(maudhui) za mwaka 2005 zinazowataka kuwasilisha ratiba ya vipindi
vyao kwa TCRA ili viidhinishwe na vilevile kuvichapisha katika gazeti kabla ya
kurushwa hewani ambapo kipindi cha Njia
Panda hakikuwasilishwa kwa ajili ya
kuidhinishwa.
Wakati huo huo, kituo cha televisheni cha Clouds
kilirusha kipindi cha ‘Bibi Bomba’ Mei 16 na Juni 6 mwaka huu kati ya saa 3.00
na saa 4.00 usiku ambacho kilikiuka kanuni za Utangazaji (maudhui) za mwaka
2005.
Alisema kipindi hicho kilidhalilisha mabibi hao
walioshiriki pamoja na wanawake kwa ujumla kutokana na maswali ya aibu
waliyokuwa wakiulizwa na waamuzi wa shindano hilo ambayo ni kinyume na kanuni
hizo.
Aidha alisema kituo hicho kinatozwa faini ya Sh milioni
moja na kutakiwa kuwasilisha TCRA
mwongozo wa kuchuja na kusimamia maudhui yasiyofaa kabla ya kutangazwa.
TCRA imesema kama Kanuni za Utangazaji zitaendelea
kukiukwa hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment