WALIMU 2,000 WA SAYANSI KUPIGWA MSASAWalimu 2,000 wa masomo ya sayansi nchini, watapatiwa mafunzo maalumu kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika kuboresha maarifa ya  ufundishaji mada ngumu katika masomo ya hesabu, fizikia na kemia.
Mradi huo ni mwendelezo wa Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP) ambao katika awamu ya kwanza ulitoa mafunzo kwa walimu 138 kwa ajili ya kufundisha masomo hayo kwa elimu ya juu na asilimia 75 ya walimu hao wamemaliza masomo na wanafundisha katika vyuo.
Akizindua mpango huo maalumu wa miezi 18 katika mikoa zaidi ya 10, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema walimu hao watakaopata mafunzo ni asilimia 20 ya walimu 10,400 wa masomo ya sayansi nchini katika sekondari.
“Wizara hii itatumia  zaidi ya dola za Marekani milioni nne kwa ajili hiyo ikiwa ni mwendelezo wa mradi huo baada ya ule wa awali kutumika kujenga uwezo kwa walimu katika vyuo vikuu sasa tunajenga uwezo kwa walimu wa sekondari,” alisema.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara  hiyo, Profesa Sylvia Temu  alisema mradi huo ni kwa ajili ya walimu, wanaofundisha masomo hayo tangu  kidato cha kwanza hadi cha nne.
Alisema mafunzo yatatolewa na taasisi nne, ambazo ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) na Chuo Kikuu cha COICT.
Mratibu wa Mradi huo Taifa, Dk Kenny Hosea alisema walimu watakaohusika, watachaguliwa kwa kutumia maofisa elimu wa wilaya ili kupata walimu 3,500, watakaochujwa na kupatikana  2,000.

No comments: