KUINUA MAISHA YA WATANZANIA SI KUMWAGA FEDHA MIFUKONI - KIKWETE



Rais Jakaya Kikwete amesema dhamira ya Serikali ni kuinua maisha ya Watanzania na dhamira hiyo iko pale pale na kwamba wanaofikiri nia hiyo ni kuwajaza wao fedha mifukoni uwezo huo haupo.
Rais alitoa kauli hiyo jana katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati akizindua ujenzi wa barabara ya Mbande  hadi Kongwa, itakayojengwa kwa kiwango cha lami.
Alisema dhamira ya Serikali ya kuinua maisha ya Watanzania haina maana kuwa wananchi watapewa fedha za kuweka mifukoni mwao.
Alisema dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo itafikiwa kwa kupitia uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, shule, njia za mawasiliano ili kurahisisha kuweza kufikia malengo yao.
“Wengine tunaposema kuinua maisha ya Watanzania wanafikiri ni kumwaga
fedha mifukoni mwao uwezo haupo,” alisema.
Pia alisema Serikali  imeboresha ukusanyaji wa fedha za ndani ili kuongeza mapato na kuondoa utegemezi katika miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete alisema makusanyo ya mapato yameongeka kutoka bilioni 170 kwa mwezi hadi bilioni 900 kwa mwezi hivi sasa na ongezeko la fedha hizo linasaidia ujenzi wa barabara za viwango vya lami na hata zile za vijijini.
Aidha alisema Serikali inafikiria  kuongeza barabara za lami mbili au tatu za ndani katika wilaya hiyo ya Kongwa.
“Tumetimiza ahadi kwenye maeneo mengi  na tunaahidi kuendeleza uwekezaji kwenye barabara, umeme na maji,” alisema.
Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli alisema mradi wa barabara kutoka Mbande  hadi Kongwa ni moja ya ahadi katika ilani ya CCM.
Alisema sehemu ya ujenzi wa barabara hiyo iliyozinduliwa ni kielelezo tosha kuwa serikali imedhamiria kujenga barabara kwa ajili ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
“Barabara hii imezinduliwa na Rais ambaye anatoka CCM na mnatakiwa kuhakikisha Rais ajaye anatoka CCM ili aendeleze kazi iliyoanzishwa haiwezekani barabara hii ije kufunguliwa na Rais wa kutoka chama kingine,” alisema.
Alisema barabara nyingi zinajengwa kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100 bila kutegemea wafadhili.
 “Tanzania ni moja ya nchi zinazojengwa barabara zenye viwango vya ndani kwa kutumia fedha zake za ndani,” alisema.
Alisema Serikali itatoa bilioni moja kwa ajli ya kusaidia ujenzi wa barabara za vijijini katika Wilaya ya Kongwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mhandisi Patrick Mfugale alisema barabara iliyozinduliwa ni sehemu ya barabara yenye urefu wa kilometa 101.7 ya kutoka Mbande hadi Kibakwe.
Alisema ujenzi wa barabara iliyozinduliwa yenye urefu wa kilometa tano asilimia 85 ya kazi yote imekamilika.

No comments: