BENKI YA DUNIA YAKUNWA NA UTEKELEZAJI MIRADI WA TANZANIA


Benki ya Dunia imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendeshwa na Serikali, inayofadhiliwa na benki hiyo.
 Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kudhamini Uwekezaji (Miga), Michael Wormser,  amesema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari. 
Alisema wanaridhika kwa sababu miradi hiyo inatekelezwa vizuri pamoja na uwazi unaoneshwa na Serikali katika utekelezaji wake. 
Baadhi ya miradi ambayo inafadhiliwa na Benki ya Dunia, ni miradi ya sayansi na teknolojia kwa elimu ya juu, huduma za afya ya msingi, utunzaji wa mazingira ya Kihansi, na mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo. 
Mingine ni pamoja na Mradi wa Uwekezaji wa Maabara za Kisasa kwa ajili ya magonjwa ya kifua kikuu katika sekta ya afya, uboreshaji wa sekta ya maji na miradi ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini. 
Wormser alitaja miradi mingine kuwa ni sekta ya usafirishaji ambayo lengo lake ni kuboresha mtandao wa barabara na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya ndege, mradi wa utunzaji wa mazingira ya Ziwa Victoria, mradi wa uboreshaji wa miji ya Zanzibar na uboreshaji wa Serikali za Mitaa. 
Pia kuna miradi ya kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuwawezesha wakulima wapate tija, kuboresha miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam ukiwemo mradi wa mabasi yaendayo kasi na Zanzibar, uboreshaji wa takwimu Tanzania pamoja na uboreshaji wa huduma za mijini. 
"Kwa kweli tunaridhishwa na utekelezaji wa miradi hii, kwa namna ambavyo inatekelezwa kwa uwazi," alisema Wormser wakati akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam. 

Katika mazungumzo yake, Makamu huyo wa Rais alisema lengo la Miga ni kusaidia uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo ya madini, miundombinu pamoja na kilimo katika nchi changa duniani, ambako wawekezaji wanakabiliwa na hatari mbalimbali  za kisiasa na mabadiliko ya mara kwa mara ya bidhaa. 
Alisema Tanzania kuna miradi ya umeme, kilimo na miundombinu, ambayo wako tayari kushirikiana na sekta binafsi, kuhakikisha wanavutia wawekezaji watakaojenga ajira na kuchangia katika ukuaji wa uchumi, ili kusaidia wawekezaji kupata faida kutokana na mchakato huo. 
"Jukumu la Miga ni kusaidia ukuaji uchumi, kupunguza umasikini na kuboresha maisha ya watu kwa kukuza uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja katika nchi zinazoendelea," alisema. 
Alitaja athari zinazokabili wawekezaji wa kigeni ambazo Miga huchukua dhamana, kuwa ni zuio la kuhamisha na kubadilisha fedha za kigeni, kutaifishwa kwa mali, vita, fujo za raia, ugaidi na hujuma, kuvunjwa kwa mkataba na kutoheshimu masharti ya fedha ya nchi huru. 
Alisisitiza kuwa Miga hutoa huduma za usuluhishi wa migogoro kwa uwekezaji uliodhaminiwa, ili kuzuia kusambaratika kwa miradi iliyo na faida ya kimaendeleo kwa nchi.\
Alipoulizwa kwa nini sekta ya kilimo haivutii wawekezaji wengi nchini, Wormser alisema ni kweli kwamba sekta ya kilimo ambayo ina fursa ya kuajiri watu wengi, inahitaji uwekezaji mkubwa na akasema kwamba taasisi yake iko tayari kudhamini wawekezaji, watakaojitokeza kuwekeza  katika eneo hilo. 
Alisema kwa sasa eneo hilo linawatisha wawekezaji wengi kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya uhakika, jambo ambalo alisema taasisi yake iko tayari kushirikiana na sekta binafsi, ili ziwekeze katika eneo la miundombinu, ambalo litasaidia kuvutia wawekezaji katika sekta ya kilimo. 
Kwa mujibu wa Wormser, bila kuhusisha sekta binafsi katika masuala ya uwekezaji, ni ngumu kupiga hatua kimaendeleo na ndio maana taasisi yake iko tayari kudhamini wawekezaji wanaoonesha nia ya kuja kuwekeza katika nchi ambazo Benki ya Dunia imeainisha kuwa mazingira yake ya uwekezaji ni tete. 
Afrika ina nchi 17, ambazo zimeainishwa na Benki ya Dunia kuwa mazingira ya uwekezaji ni tete, kutokana na kugubikwa na migogoro inayoogopesha wawekezaji, kwa vile wanahofia hatari za kufanya biashara katika nchi hizo na usalama ni mdogo kisiasa kuliko faida ya kuingia kwenye masoko yenye faida kubwa.

No comments: