MTAMBO WA KIHANSI WAPOTEZA SHILINGI BILIONI 34



Mtambo wa kuzalisha umeme unaotumia maji wa Kihansi, umepoteza takribani Sh bilioni 34 kipindi cha masika, kutokana na udogo wa bwawa lililopo la kuhifadhia maji hayo na hivyo kulazimika kuyamwaga.
Kiasi hicho cha fedha kimepotea kati ya Machi na Mei mwaka huu, ambapo bwawa hilo dogo lililopo Kihansi chini, lilijaa na kushindwa kuhimili maji hayo na kulazimika kuyamwaga maeneo mengine na kupotea bila kutumika.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mtambo huo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, aliyetembelea mtambo huo jana, Meneja wa Mtambo wa Kihansi, Pakaya Mtamakaya, alisema ili kuondokana na hasara hiyo, ni vyema kukajengwa mabwawa ya kuhifadhia maji hayo na kuongeza mitambo miwili ya kuzalishia zaidi umeme.
“Endapo kungekuwa na mabwawa mengine ya kuhifadhia maji kipindi cha masika, tungeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, kwani maji haya yanayopotea yangetuwezesha katika kipindi hicho cha Machi hadi Mei, kuzalisha uniti za umeme takribani milioni 129 ambazo zingetupatia takribani Sh bilioni 34,” alisema Mtamakaya.
Alisema Kihansi katika matarajio yake imejiwekea malengo ya kuchimba mashimo ya kusimika mashine mbili za kuzalisha umeme lakini pia mkakati wa kuanzisha mabwawa yatakayosaidia kuhifadhi maji  wakati wa masika ili yasipotee.
“Mkakati wa haraka ni kufunga mashine hizo mbili ambazo mashimo yake yako tayari, mashine hizo zitasaidia kutumia maji hayo katika kipindi cha masika lakini pia zitakuwa kama za dharura pindi itakapotokea uhitaji mkubwa na hivyo kufanya Kihansi kuwa na mashine tano za kuzalisha umeme badala ya tatu zilizopo sasa,” alisema.
Alisema kwa sasa mtambo huo unazalisha uniti 120,000 kwa mwezi na hutumia Sh milioni 200 kama gharama za uendeshaji na umeme unapozalishwa huuzwa kwa Sh tano kwa watumiaji.
Aidha alisema kwa sasa kituo cha mtambo huo kinakabiliwa na changamoto ya miundombinu kutokana na kuzungukwa na barabara mbovu pande zote kiasi cha kusababisha kisifikike hasa kipindi cha masika na kusababisha kuwepo na ugumu wa utendaji katika kipindi hicho.
Katibu Mkuu, Maswi, alisema wajibu wa Serikali katika kuendeleza mtambo huo ni kusaidia ujenzi wa mashine hizo, ambazo zikifungwa zitazalisha megawati 120 na kuingiza zaidi ya Sh bilioni 120 lakini pia zitasaidia kutopoteza kiasi kikubwa cha maji kama ilivyo sasa.

No comments: