Kampuni ya Maendeleo ya mafuta ya China (CNPC)
inayosimamia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara - Dar es Salaam imetoa
msaada wa boti ya kubeba wagonjwa kwa wananchi wa kisiwa cha Songosongo
kilichopo Kilwa mkoani Lindi.
Pia wametoa msaada wa viatu jozi 240, jezi za mpira 30
pamoja na mipira 10 kwa ajili ya mpira wa miguu kwa shule ya msingi Songosongo,
vyote vikiwa na thamani ya dola za Marekani 65,000 (Sh milioni 105).
Akikabidhi msaada huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni
hiyo, Mao Qiping alisema misaada hiyo ni shukrani kwa wakazi wa kisiwa hicho
kwa ukarimu waliouonesha tangu walipoanza kazi ya ujenzi wa bomba hilo mpaka
sasa linapotarajia kukamilika.
Alisema urafiki kati ya nchi hiyo na Tanzania ni wa muda
kuanzia ujenzi wa reli ya TAZARA mpaka sasa wanapojenga bomba hilo ambalo ni
mkombozi wa tatizo la umeme nchini jambo litakalosaidia kuinua uchumi wa nchi.
Akishukuru kwa msaada huo mara baada ya kukabidhiwa
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Abdallah Yahya
alisema msaada huo utasaidia kuwa na usafiri wa uhakika kwa wagonjwa
kutokana na sasa kutumia mashua ambazo ni hatari kwa maisha.
Jambo lililoungwa mkono na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule
ya Msingi Songosongo, Haji Njechele alisema boti hiyo itasaidia kupunguza vifo
ambavyo vilikuwa vikitokea kutokana na kukosekana usafiri.
No comments:
Post a Comment