MENEJIMENTI INAYOJENGA KIWANDA CHA DANGOTE YAWASHIWA MOTO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ameijia juu menejimenti inayosimamia ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote, kwa kutowapatia fursa wahandisi wazawa kushiriki katika ujenzi na uendeshwaji wa mradi huo.
Pia alionesha kushangazwa na hatua ya uongozi wa kiwanda hicho kufikiria kuagiza makaa ya mawe kutoka Msumbiji, wakati Tanzania ina rasilimali hiyo katika maeneo kadhaa nchini. 
Akizungumzia suala la ushirikishwaji wa wahandisi wa kizalendo na ajira za watanzania katika mradi huo, Maswi alisema ni lazima kiwanda hicho kuwa na wataalamu wazawa watakaojifunza na kujua mambo yanayoendelea katika mradi huo, kwa kuwa wao ndio baadae watakaouendesha. 
Maswi aliyasema hayo juzi alipotembelea kiwanda hicho na kuzungumza na uongozi unaosimamia mradi huo kutoka kampuni ya India ya Sinoma International Engineering Co. Ltd.
Katika mazungumzo hayo alianza kuihoji menejimenti hiyo juu ya mipango na mikakati yake katika kuhakikisha watanzania wananufaika na mradi huo katika maeneo ya ajira na utaalamu, ambapo majibu ya uongozi huo hayakumridhisha. 
Akizungumza kwa hasira, Maswi alisema serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya aina hiyo na kuwataka kubadilika mara moja. 
Menejimenti inayosimamia mradi huo ina jumla ya wasimamizi 12 kutoka katika kampuni hiyo pekee na wote ni raia wa India huku wazawa wanaoishiriki katika mradi huo wakiwa ni vibarua pekee. 
Kiwanda hicho kinachotarajiwa kuanza uzalishaji mwakani, kitakuwa kinatumia gesi inayozalishwa na kuchakatwa katika kituo cha Madimba mkoani hapa.
Akijibu maswali ya Maswi kuhusu suala la ajira, Meneja Mradi wa Dangote, Daljit Singh alikiri kuwa hakuna wahandisi wazawa walioshirikishwa katika ujenzi wa mradi huo isipokuwa tayari kiwanda hicho kimetangaza nafasi za kazi na hadi sasa walioomba ni watu 700 ambao ni kwa ajili ya kazi za kiufundi.
Kuhusu suala la makaa ya mawe, Maswi alisema alipata taarifa hizo baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya ziara nchini Nigeria na kukutana na mmiliki wa kiwanda hicho, Alhaji Aliko Dangote kuwa menejimenti ya kiwanda hicho iko kwenye mazungumzo na Msumbiji kwa ajili ya kununua makaa hayo ya mawe. 
Aliwashauri kufanya mazungumzo na serikali kuangalia uwezekano wa kuomba kibali cha kupata makaa ya mawe hapa nchini ambayo yanapatikana kwa wingi katika maeneo ya Mchuchuma, Liganga, Kiwira na Ngaka. 

No comments: