MTUHUMIWA KESI YA SWISSPORT ALALAMIKIA UNYAMA POLISI


Kesi ya wizi wa simu inayowakabili wafanyakazi sita wa Kampuni ya Kupakia na Kupakua mizigo ya Swissport, imechukua sura mpya baada ya mshitakiwa Hashim Idd (49) kudai amefanyiwa vitendo vya unyama alipokuwa anachukuliwa maelezo na Polisi. 
Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya ya Ilala imepokea kama kielelezo maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo baada ya kukataa maelezo yaliyotolewa  mahakamani hapo kama kielelezo, kwa madai kuwa alilazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyatoa polisi wakati akihojiwa. 
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Juma, Idd alidai mbali na kulazimishwa kusaini maelezo hayo aliingiziwa chupa sehemu ya haja kubwa na askari polisi walikuwepo katika chumba ambacho alikuwa akichukuliwa maelezo katika kituo cha polisi cha Uwanja wa ndege ili aweze kukubali mashitaka hayo ya wizi. 
Hata hivyo, mahakama hiyo iliyakataa  maelezo hayo kwa madai kuwa ni maelezo ya kutunga na hayana ushahidi.  
Katika kesi hiyo, shahidi Phraim alidai kuwa siku ya tukio, Januari 31 mwaka huu alipewa taarifa za kesi ya wizi wa simu kutoka kwa mkuu wa upelelezi wa kituo hicho.  
Alidai wizi huo ulitokea Januari 27 mwaka huu, saa 7:10 mchana  ambapo boksi moja lenye simu 460 aina ya Tecno na Itel liliibwa kutoka katika ndege ya Qatar Airways iliyokuwa ikitoka nchini China.  
Washitakiwa hao ni Hamada Mohammed (42), Haji Waziri (26), Yusuph Muhangwa (33), Hashimu Idd (49), Ally Omary (33) na Hamisi Othuman (29) ambao walituhumiwa kuiba simu zenye thamani ya Sh milioni 19.4 mali ya Chemchem. Washitakiwa wapo nje kwa dhamana.

No comments: