Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), inatarajia kukabidhi
madawati 2,000 kwa shule za msingi 10 zilizopo jijini Dar es Salaam katika
kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati nchini.
Hayo yamesemwa na Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa
mamlaka hiyo, Sylvia Lupembe wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam jana.
“Wanafunzi zaidi ya 6,000 watanufaika na madawati hayo
ambayo yatagharimu zaidi ya Sh milioni 150,” alisema Lupembe.
Akifafanua, Lupembe amesema shule zitakazonufaika ni
Chamazi, Mbande, Boko NHC, King’ong’o, Hekima, Bwawani, Bunju, Goba, Kombo na
Kingugi.
Pia Lupembe alibainisha kuwa tathmini ya mwaka 2013
Tanzania ina upungufu wa madawati 1,147,471 hivyo ni jukumu la kila mdau kuunga
mkono juhudi hizo ili kuondoa tatizo hilo kote nchini.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa Benki ya
KCB, Christina Manyenye amesema wamekuwa wakishiriki katika kuchangia madawati
ambapo kwa mwaka jana walichangia zaidi ya madawati 700.
TEA kwa kushirikiana na Kampuni ya Mafuta ya TOTAL na
wadau wengine kama Kenya Commercial Bank
(KCB), na Social Action Fund
wamekuwa katika ushirikiano tangu mwaka 2013 katika kutatua changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu nchini.
No comments:
Post a Comment