VITUO VYA USHAURI KWA WATOTO VYATENGEWA FEDHA

Serikali imetenga fedha kwa ajili ya vituo vyote vinavyotoa ushauri na kurekebisha watoto walio chini ya umri wa miaka 18 vilivyo chini ya Idara ya Ustawi wa jamii nchini.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,  Nsachris Mwamwaja alitoa taarifa hiyo kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti moja la kila siku lililokuwa na habari  iliyosema mahabusu ya watoto inadaiwa Sh milioni moja.
“Ni kweli tatizo hilo lipo ndiyo maana Serikali imetenga fedha tayari ambazo zitagawiwa kwenye vituo vyote nchi nzima,” alisema Mwamwaja (pichani).
Mwamwaja ambaye hata hivyo hakutaja ni kiasi gani cha fedha kilichotengwa na Serikali kwa ajili hiyo, alisisitiza kuwa deni hilo litalipwa kwenye mahabusi hiyo iliyoko Tanga.
Mahabusi hiyo ni miongoni mwa vituo kadhaa vilivyo chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii ndani ya Wizara ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Matumizi ya fedha hizo ni pamoja na kushughulikia tatizo la maji na uhaba wa chakula kituoni hapo kuendelea kutoa huduma stahiki kwa watoto hao na kufikia lengo la kuwarekebisha tabia zao ili wawe raia wema nchini. 
Aidha, Mwamwaja alisema fedha zilizotengwa si za Mkoa wa Tanga pekee bali ni kwa ajili ya vituo vya nchi nzima zikiwemo kambi za wazee wasiojiweza, mahabusi za watoto na kambi za kutibu wagonjwa wa ukoma.

No comments: