MAGONJWA YA AKILI SASA TISHIO KWA VIJANA

Asilimia 61 ya wagonjwa wa akili katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza inasadikiwa kuwa ni vijana, hali ambayo imeelezwa inachangia ongezeko la umasikini katika jamii.
Mratibu wa Magonjwa ya Akili wa wilaya hiyo, Madoshi Shemu  aliwaambia wakazi wa Kijiji cha Mriti jana kuwa juhudi za pamoja zinahitajika kuokoa kundi hilo muhimu kwa uchumi na maendeleo ya taifa.
Alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Shirika la Forum Syd kijijini hapo katika kilele cha siku ya vijana.
Kwa mujibu wa Shemu, kati ya wagonjwa wa akili 266 waliopokewa mwaka jana katika hospitali ya wilaya hiyo, 166 ni vijana.
Alisema mbali ya ugonjwa wa kifafa kuathiri idadi kubwa ya  wagonjwa wa akili katika wilaya hiyo, pia dawa za kulevya hasa  bangi zinachangia tatizo hilo kuwa kubwa. Mengine yanayochangia tatizo ni sigara na ugoro.
Alisisitiza umuhimu wa jamii kutambua magonjwa hayo hususani kifafa, yanatibika hospitalini.
Mratibu wa Shirika la Forum Syd wilayani Ukerewe, Sophia Donard  alisema wameguswa na tatizo hilo la afya ya akili  kwa vijana.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, tafiti mbali mbali zinaonesha kuwa  asilimia 20 ya  vijana wote duniani, wanapatwa tatizo la afya  ya akili. Alisema kati ya hao, asilimia 85 wanaishi katika nchi masikini  ikiwemo Tanzania.

No comments: