MBINGA YAPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI

Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imefanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito kutoka  79 kati ya 100,000 mwaka 2010 hadi 65 mwaka 2013 hatua iliyotokana na kutekeleza mkakati wake wa kupunguza vifo vya uzazi.
Aidha, katika mkakati huo pia imeweza kupunguza idadi ya vifo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka wastani wa vifo 16 kati ya 1,000 mwaka 2010 hadi vifo 10 mwaka 2013. Lengo ni kufikia angalau watoto 5 ama kumaliza kabisa ifikapo mwakani.
Hayo yalisemwa jana na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Damas Kayera wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea namna wilaya hiyo ilivyojipanga katika kuboresha huduma zake za afya.
Dk Kayera alisema kuwa, kupitia Mpango wa  Afya ya Msingi (MMAM) katika bajeti ya mwaka 2014/15, halmashauri inajenga zahanati 15 kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.
Alisema wamelazimika kuimarisha na kuboresha huduma hizo kutokana na ongezeko kubwa la watu katika wilaya hiyo ambao wanahitaji kupatiwa huduma za matibabu kutoka 353,683 mwaka 2012 hadi kufikia 374,493 sawa na ongezeko la asilimia 2.9.
Katika mkakati huo, tayari serikali imeshajenga nyumba sita za waganga katika Zahanati ya Mkako, Lihale, Litumbandyosi, na Tukuzi ambazo zinatarajia kumalizika hivi karibuni na kutoa fursa kwa watumishi wa idara hiyo kuwa na makazi bora.
Hata hivyo, alisema licha ya mafanikio hayo bado idara hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji nguvu ya pamoja kuzimaliza, ikiwamo upungufu wa watumishi wenye taaluma ya udaktari na uuguzi na magari ya kubeba wagonjwa.

No comments: