UNILEVER TANZANIA WAZALISHA AJIRA ELFU SABA

Kampuni ya Unilever Tanzania Limited imesema kutokana na Tanzania kuwa soko kubwa la bidhaa zao wametoa ajira kwa watu 7,000 kwa kuwekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 70 (Sh bilioni 112).
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo  Afrika Mashariki, Marc Engel alisema  hayo jana wakati wa uzinduzi wa toleo jipya la sabuni ya OMO uliofanywa na Mke wa Makamu wa Rais, Asha Bilal.
Alisema  kwa kutambua shughuli nyingi zinazowakabili wanawake majumbani, sabuni hiyo ni suluhisho lao kwani inasafisha nguo kwa dakika moja na kuwataka wazazi wasiwakataze watoto kucheza kwamba watachafuka kwani pia wanajifunza na kugundua vitu mbalimbali.
“Uchafu ni mzuri, akinamama wa Kitanzania sasa wanaweza kuwapa watoto uhuru wa kucheza na kujifunza bila kuwa na wasiwasi wa nguo kubaki madoa sugu baada ya kufuliwa,” alisema Engel.
Akizungumza, Mama Bilal aliipongeza kampuni hiyo kwa jitihada zao katika kuboresha maisha ya kinamama na watoto siku hadi siku na uboreshaji wa sabuni hiyo kuwawezesha kufua kwa muda mfupi na kupata nafasi ya kushiriki shughuli za maendeleo.
“Katika ulimwengu wa sasa, mwanamke hakai nyumbani tu kama ‘golikipa’, mimi kama mama, naelewa kuna changamoto nyingi za kifamilia lakini nahamasisha kinamama tuamke , tupambane kuimarisha nafasi yetu katika familia na jamii kwa ujumla,” alisema Mama Bilal.

No comments: