Rais Jakaya Kikwete amewaonya viongozi wa ngazi mbalimbali nchini, wakiwemo wa Halmashauri kuacha mara moja tabia ya kujigeuza kuwa madalali wa kuuza mapori ya ardhi, bali wazingatie suala la umuhimu wa kuweka akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Pia amewataka viongozi wa Halmashauri hizo za wilaya nchini kuweka utaratibu wa kupima viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, na kuacha tabia ya kujilimbikizia viwanja, bali wawe na uwazi kwa wananchi kuhusu suala zima la ugawaji wa viwanja vinavyopimwa ili kuondoa manung’uniko ya wananchi.
Rais alisema hayo kwenye hotuba yake ya majumuisho yaliyofanyika juzi katika ukumbi wa Sekondari ya Gairo akihitimisha ziara yake ya wiki moja mkoani Morogoro aliyoianza Agosti 20 mwaka huu na kuzitembelea wilaya zote sita za mkoa huo.
Katika kusimamia matumizi bora ya ardhi, Rais Kikwete aliwaagiza viongozi wa Halmashauri za wilaya kuwajibika kuhakikisha mapori ya ardhi yaliyopo katika maeneo yao yanahifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na si kuendelea kuyauza.
Rais alisema kuwa si kila eneo la ardhi isiyotumika itumike yote kwa sasa, na kwamba haiwezekani ardhi yote iliyopo inaweza kulimwa hivi sasa, bali ni budi iendelee kuwekwa akiba kwa vizazi vijavyo.
“Mkianza kugawa ardhi yote ambayo mnayoiona ni mapori mtawakosesha watakaokuja kwa maana kizazi kijacho, hakitakuwa na ardhi ya kutumia...kama mababu zetu wangekuwa na mawazo ya kutumia ardhi yote , kizazi cha sasa hiki chetu kisingekuwa na ardhi ya kutumia,” alisema Rais.
Rais Kikwete aliwataka viongozi wa serikali za wilaya na mkoa kuwa wepesi wa kutatua matatizo ya wananchi yanayohusu ardhi ili kuepusha ugomvi na kuwa wajibu wa kuyafanyia kazi kwa haraka migogoro inapoibuka kwa kuwapatia majawabu sahihi ili kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi.
Hivyo aliwataka viongozi wa serikali za vijiji kuzingatia matumizi bora ya ardhi ikiwa na kilimo, mifugo, makazi na maeneo ya akiba kwa ajili ya watoto wao.
No comments:
Post a Comment