BABU WA MIAKA 90 ATEKETEA KWA MOTO AKIWA USINGIZINI


Mkazi wa Kimara Temboni, Felix Makundi (90) amekufa papo hapo baada ya kuteketea kwa moto wakati akiwa amelala. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kuwa mzee huyo aliteketea juzi baada ya moto kuzuka katika nyumba yenye vyumba vitatu mali ya Benson Makundi na kumuunguza mzee huyo mwili mzima hadi kufa pamoja na kuteketeza mali zote zilizokuwamo ndani. 
Alisema wakati moto huo unatokea, mwenye nyumba hakuwepo na hadi sasa chanzo cha moto huo hakijafahamika. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha huku Polisi wakiendelea na upelelezi wa tukio hilo. 
Wakati huo huo, fundi umeme wa kampuni ya Catic, Omari Mkula (35), amekufa papo hapo baada ya kudondoka kutoka ghorofa ya nne wakati akiendelea na ujenzi. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya wa Kihenya alisema kuwa fundi huyo alikufa juzi mchana katika eneo la Tuangoma, Temeke katika Mradi wa NSSF baada ya kudondoka kutoka ghorofa ya nne baada ya kamba ya winchi kukatika. 
Kamanda Kihenya alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Temeke kwa uchunguzi zaidi. 

No comments: