Watu kumi
akiwemo mama na mtoto wake wamekufa papo
hapo na wengine wanane kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace waliyokuwa
wanasafiria kugongana na lori katika mji mdogo wa Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Ajali hiyo
imetokea majira ya saa 6:00 mchana
imehusisha gari aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea Jijini Mbeya
na Fuso lililokuwa likitokea katika kituo cha mafuta na kuingia barabara kuu ya
kutoka Mbeya kwenda Tunduma.
Akizungumzia
ajali hiyo, Muuguzi Mkuu wa Hospitali teule ya wilaya ya Mbeya, Sikitu Mbilinyi
alisema kuwa wamepokea maiti 10 wakiwemo
wanawake wanne, wanaume wanne na watoto
wawili.
Alisema katika
majeruhi wanane waliopokelewa hospitalini hapo, watano ni wanaume na watatu ni wanawake na kwamba
madaktari baada ya kubaini hali za majeruhi hao kuwa mbaya walishauri wapelekwe
katika hospitali ya rufaa Mbeya .Tayari majeruhi watatu akiwemo mwanamke mmoja
wamehamishiwa katika hospitali hiyo.
Aliwataja
waliokufa katika ajali hiyo ambao wametambuliwa na ndugu zao kuwa ni pamoja na
Mariam Mashambwe na mtoto wake Hamis Chaula, Rebeca Keneth, Petro mgogo, Haruna
Jamison na Martin Mwasolikoto.
Aliwataja
majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo na kulazwa kuwa ni pamoja na
kondakta wa Hiace, Justin
Chaula(28)mkazi wa Mabatini, kondakta wa lori Joseph Stephano (22) mkazi wa Mbalizi , aliyekuwa abiria wa roli
Ziona Goa (20), Newton Patrick na dereva
wa lori, Amoni Mwakoko.
Mmoja wa
majeruhi wa ajali hiyo, Ziona Goa
alisema kuwa Hiace waliyokuwa wamepanda ilikuwa na hitilafu katika breki na
kusababisha gari kwenda kwa mwendo wa kasi na dereva kushindwa kulidhibiti na
kuligonga lori ambalo tayari lilikuwa limeingia barabarani.
“Tulimsikia
dereva akisema breki hazifanyi kazi huku gari likiwa kwenye mwendo kasi na
ghafla mbele yetu kukawa na lori limekwisha ingia barabarani na tukaligonga
ubavuni,” alisema.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na
kwamba uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment