Suala la uraia pacha limeonekana ‘kupigwa chini’ na serikali na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya wote kukubaliana zaidi juu ya hasara za kuruhusu uraia huo, ikiwemo hofu ya usalama wa taifa na uzalendo kupungua.
Katika semina iliyoandaliwa kwa Wajumbe wa Bunge hilo na mada kutolewa na Idara ya Uhamiaji, Abdallah Khamis Abdallah ambaye ni Kamishna wa Udhibiti na Mipaka wa idara hiyo, imeonesha kuruhusiwa uraia pacha ni hasara zaidi kwa Tanzania kuliko faida.
Suala hilo kwenye semina hiyo likawafanya wajumbe zaidi ya 12 kati ya 16 waliochangia kukataa uraia pacha na kumuacha mwakilishi wa Diaspora, Kadari Singo kutumia nguvu nyingi kutetea uraia pacha huo.
Wajumbe wa Bunge wakizungumza na mwandishi wameeleza kuwa Uhamiaji imeeleza kuwa Watanzania wameondoka nchini kwa sababu za kufuata elimu, viapo vilivyowafanya wawe watiifu kwa nchi walizopata uraia na wengine kwa kuitukana nchi haifai na hawawezi kuishi Tanzania.
Mjumbe Wazir Rajab Salum alisema Uhamiaji imetaja faida ya uraia pacha ni za kiuchumi pekee na nyingi ni hasara, ikiwemo kuangalia uzalendo ambapo imeonekana kuruhusu kutapunguza uzalendo na usalama wa taifa utakuwa hatarini.
“Kumeonekana yule mtanzania aliyeapa kuilinda nchi ya pili iliyompa uraia mwingine ni rahisi kumtumia kuifanyia ubaya Tanzania na walioondoka wameonekana wanakosa uzalendo hata akirudi hawezi kuwa sawa na Mtanzania aliyebaki nchini miaka yote,” alieleza Salum.
Hata hivyo, aliongeza; “wapo waliounga mkono uraia pacha lakini wakataka watanzania waliochukua uraia nje wawekewe utaratibu wakipewa uraia nchini wasiruhusiwe kushiriki nafasi za uongozi yaani wasichague wala kuchaguliwa”.
Naye Almas Maige alisema Uhamiaji imeona waliokula viapo nje vya uraia hawataweza kutumikia ‘mabwana’ wawili na tayari wameshaonekana si waaminifu kwa nchi yao ya awali.
Hata hivyo, Singo akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge alitetea hoja yake ya Tanzania kuruhusu uraia pacha na kusema, “wanasema aliyeomba uraia wa nje amekosa uzalendo hivi mzalendo ni yupi anayeiibia pesa nchi akapeleka nje au anayeleta pesa nchini. Uzalendo si kigezo kwani mtu yeyote anaweza kukosa uzalendo…”
“Usalama wa taifa wanaosema unahatarishwa ni upi ni kwa mtanzania aliye nje kuja nchini kwake au kumpa uraia wa pili Mnyarwanda ambaye nchi yake inaruhusu uraia pacha na ukamnyang’anya hati ya kusafiria na akienda kwao atapewa nyingine huku akitoa siri za nchi na yule mfanyakazi wa serikali mwenye siri nyingi anayezitoa kwa kupokea rushwa. Marekani inaweza kuleta satelaiti ikasikiliza mawasiliano ya nchini. Hivi si vigezo vya kumnyima uraia mtanzania aliye nje”.
Akitoa mifano ya faida kwa nchi zilizoruhusu uraia pacha, alisema Wachina waliopo nje wanarudisha kwao dola za Marekani bilioni 60 kwa mwaka, Nigeria dola za Marekani bilioni 20 na Kenya inapata dola za kimarekani bilioni 1.7 kutoka kwa Wakenya waliopo Diaspora.
Kwa sasa watanzania waliopo wanaleta nchini dola za kimarekani kati ya milioni 10 na 37 huku Benki ya Dunia ikionesha watanzania waliopo nje ni milioni tatu.
Alishauri uraia pacha uruhusiwe na kuwekwe mipaka, kwani hata yeye na watanzania waliopo nje wanajua hawawezi kurejeshewa uraia wao kwa asilimia 100. Tanzania ni kati ya nchi saba za Afrika ambazo hazijaruhusu uraia pacha. Burundi ni miongoni mwao.
Katika semina hiyo Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Dk Philip Mpango aliwaeleza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba umuhimu wa kuweka mpango mkakati wa uchumi imara kwenye rasimu ya katiba mpya na kuwekwe uhakika wa viwanda endelevu.
No comments:
Post a Comment