Serikali imetenga jumla ya Sh milioni 287 kuwalipa fidia wananchi
wa vijiji 5 karibu na hifadhi ya wanyama Serengeti upande wa Wilaya ya Tarime
mkoani Mara.
Fidia hiyo inatokana na uharibifu uliofanywa na wanyamapori kwa
mazao yao shambani.
Vijiji vinavyohusika ni pamoja na Nyarukoba, Nyanungu , Gorong'a ,
Kemambo na Kegonga.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Tarime Silvanus Gwiboha wakati akijibu maswali ya madiwani kuhusiana na
suala la fidia kutoka serikalini baada ya tembo kufanya uharibifu mkubwa katika
mashamba ya vijiji hivyo.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya
Tarime kilichofanyika hapo Agosti 27
katika ukumbi wa Halmashauri hiyo chini ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo Selvester Kisyeri Kaimu Mkurugenzi huyo alisema fedha hizo zilipatikana
kutokana na juhudi kubwa ya Mbunge Nyambari Nyangweni aliyewasilisha suala hilo
bungeni na Serikali kutoa ahadi ya kulipa fidia.
Mkurugenzi huyo alisema kitu wanachofanya sasa ni kuhakiki majina
kwani yapo madai kuwa kuna watu wanafanya hila ya kudhulumu Serikali kwa
kuandikisha majina hewa.
Wakati huo huo Baraza la Madiwani limewataka maofisa wa Kilimo
kukabiliana na ugonjwa wa mnyauko na kubabuka mazao ya mahindi.
Ugonjwa huo umebainika kuwapo katika kata zaidi ya 15 za Nyarero,
Nyanungu, Kitare, Turwa , Pemba , Nyamaraga , Nyandoto, Nyamisangura, Kibasuka,
Nyakonga, Kemambo, Nyamwaga na Mbogi .
Imedaiwa kwamba ugonjwa huo umeathiri asilimia 25 ya zao la mahindi.
No comments:
Post a Comment