Tanzania imekuwa ikipoteza tani 18 za dhahabu kila mwaka, zenye
thamani ya zaidi ya Sh trilioni moja, kutokana na ujanja wa wawekezaji katika
uchimbaji wa madini.
Imeelezwa kuwa watu hao huenda kinyume na taratibu za wachimbaji
wadogo, katika kuchimba na kuuza madini hayo wakifanya hivyo kwa hila bila
kutambuliwa rasmi.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Madini Tanzania, Paul Masanja,
ambaye aliongeza kuwa utaratibu huo unaotumiwa na wawekezaji ni wa kienyeji na
unalitia Taifa hasara kubwa kutokana na madini mengi kupotea.
“Pamoja na wachimbaji hawa kulaliwa na wanunuzi wajanja kutokana
na kutojua bei halisi ya madini, pia wamekuwa wakisababisha upotevu mkubwa wa
madini yetu, ambapo kwa upande wa dhahabu jumla ya tani 18 hupotea kutokana na
utaratibu huo wa kienyeji,” alisema Masanja.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imeanzisha utaratibu wa
kuwatambua rasmi wachimbaji wadogo kwa kuwapatia ruzuku za kujiendeleza kupitia
vikundi ambapo hadi sasa wachimbaji 11 wameshapatiwa ruzuku hizo takribani dola
558,000.
Aidha alisema kwa sasa Serikali haiwezi kuruhusu wachimbaji hao
wadogo kuuza madini kwa kutumia dola ili wapate faida kama wanavyodai kwa kuwa
kitendo hicho kitaiua Shilingi ya Tanzania.
“Hata hivyo, hili ni soko huria hatuwezi kupangia mtu bei ya kuuza
madini kwa kuwa kwa sasa tuna soko huria lakini ili nchi yetu iwe salama,
madini hayafai kuuzwa kwa dola,” alisema Masanja.
Hivi karibuni akiwa wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, baadhi ya
wachimbaji wadogo walimtaka Katibu Mkuu, aingilie kati na kuwasaidia
watambulike rasmi katika biashara hiyo ya madini ikiwa ni pamoja na kuruhusiwa
kuuza madini hayo kwa dola za Marekani ili wapate faida.
No comments:
Post a Comment