MWEKEZAJI AAGIZWA KUJENGA MTAMBO WA KUZALISHA UMEME



Serikali imetaka mwekezaji katika Mgodi wa Chuma wa Liganga na wa Makaa ya Mawe Mchuchuma, Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL), kuanzisha mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.
Katika hilo, imemtaka mwekezaji huyo kurejea upya mapendekezo yao ya kuanzisha kuhusu gharama, kwa kuwa gharama ya kuzalisha umeme iliyopendekezwa haiendani na viwango vya kimataifa.
Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wakati alipotembelea migodi hiyo, iliyopo wilayani Ludewa, mkoani Njombe juzi.
Katika ziara hiyo, wawekezaji hao walimtaka aingilie kati ili mtambo huo uanzishwe mapema kutokana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushindwa kufikia nao muafaka.
“Hata katika nchi nyingine maendeleo kama haya yakifanyika, ujenzi wa laini za kusafirishia umeme kilometa moja inatozwa kama dola za Marekani 170,000 hivi, lakini hawa wenzetu katika mapendekezo yao wanataka ujenzi wa laini hizo kilometa moja, ifikie dola za Marekani milioni moja, mliona wapi? Hili haliwezekani,” alisisitiza Maswi.
Alisema kama hiyo haitoshi katika mapendekezo yao ya awali kwa Tanesco, walipendekeza bei ya kuwauzia umeme Tanesco ya dola za Marekani senti 12 kwa uniti moja, kiwango ambacho ni cha juu kutokana na ukweli kuwa watatumia makaa ya mawe mali ya Watanzania kuzalishia umeme huo.
Alisema endapo wataleta mapendekezo yanayokubalika yenye kuzingatia maslahi ya pande zote mbili, Serikali haina pingamizi lolote la ujenzi wa mtambo huo na itatoa ushirikiano ili kuufanikisha kwa kuwa utamaliza matatizo ya umeme katika maeneo ya Ludewa, Njombe, Makambako na huenda na nchi jirani.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya migodi hiyo mbele ya Katibu Mkuu, Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCIMRL, Eric Mwingira, alimuomba Katibu Mkuu huyo aingilie kati na kusaidia kuwepo na maelewano baina ya wawekezaji hao na Tanesco ili kuwezesha kujenga mtambo huo wa umeme utakaozalisha megawati 600.

No comments: